Mdahalo wa kwanza wa wagombea urais Iran wafanyika
Wagombea sita wa uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alasiri ya leo wameshiriki katika mdahalo wa kwanza wa moja kwa moja katika kanali ya kwanza ya televisheni ya taifa.
Mdahalo huo ambao pia umerushwa moja kwa moja hewani kote duniani kupitia kanali ya televisheni ya Kiingereza ya Press TV, leo umehusu masuala ya kijamii ambapo midahalo miwili itakayofuata itahusu masuala ya kiuchumi na kisiasa.
Wagombea hao sita wamepata fursa ya kubainisha mitazamo yao na pia wameulizwa maswali na wagombea wengine katika mdahalo huo.
Wagombea sita wa urais mwaka huu ni pamoja na Mostafa Aqa-Mirsalim ambaye ni waziri wa zamani wa utamaduni na muongozo wa Kiislamu, Mostafa Hashemi-Taba makamu wa rais wa zamani ambaye pia aliwahi kuwa mkuu wa kamati ya taifa ya Olimpiki, Es'haq Jahangiri makamu wa kwanza wa serikali ya sasa, Mohammad-Baqer Qalibaf meya wa mji wa Tehran, Seyyed Ebrahim Raeisi msimamizi wa Haram Takatifu ya Imam Ridha AS na rais wa hivi sasa, Hassan Rouhani ambaye anatetea nafasi yake ili amalize kipindi chake cha pili.
Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe 19 mwezi ujao wa Mei sambamba na uchaguzi wa tano wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji kote nchini Iran.