Qassemi: Kikao cha Marekani na Waarabu mjini Riyadh ni njama za Kizayuni
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria safari ijayo ya Rais Donald Trump wa Marekani nchini Saudia kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa nchi za Kiarabu na Marekani mjini Riyadh na kusema kuwa, kufanyika kikao hicho ni katika njama za Wazayuni.
Mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz Aal Saud hivi karibuni aliwatumia barua wakuu wa nchi 17 kwenda kuonana na Donald Trump, wakati rais huyo wa Marekani atakapokuwa ziarani nchini Saudia.
Rais wa Marekani anatarajiwa kuitembea Saudia tarehe 23 mwezi huu. Akizungumzia safari hiyo, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hiyo ni njama ya Wazayuni ambapo kwa kuzingatia uhusiano uliopo baina ya Saudia na Israel, Riyadh imekipa jina jinghine kikao hicho ili kufunika na kutodhihirisha uhusiano huo.
Amesema, matatizo ya ndani ya Saudia, hujuma yake ya kivita huko Yemen na kuhisi kutengwa Riyadh ni baadhi ya mambo yaliyousukuma utawala wa Aal Saud kuitisha kikao hicho.
Itakumbukwa kuwa, viongozi walioalikwa kutembelea Saudi Arabia wakati wa ziara hiyo ya Donald Trump ni pamoja na mtawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mfalme wa Bahrain, Amir wa Qatar, Amir wa Kuwait na Rais wa Uturuki. Mfalme wa Saudia amewaalika viongozi hao kutembelea Riyadh wakati wa ziara ya Rais Donald Trump kwa madai ya kushiriki kikao cha eti nchi za Kiarabu - Kiislamu na Marekani.