Hauli ya Imam Khomeini (MA) kufanyika kesho; Kiongozi Muadhamu atahutubia waombolezaji
Hauli ya mwaka wa 28 tangu alipoaga dunia mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (MA) itafanyika kesho kwenye haram ya kiongozi huyo ambapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei anatazamiwa kuhutubia umma wa wananchi watakaohudhuria hauli hiyo.
Kamati ya maandalizi ya hauli ya Imam Khomeini (MA) imetangaza kupitia taarifa kuwa hauli ya mwaka wa 28 tangu alipoaga dunia Imam Khomeini itafanyika kesho Jumapili saa 12 jioni kwenye haram toharifu ya mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maeneo ya kandokando ya haram hiyo.
Visomo vya Qur'ani vitakavyoongozwa na maqarii mashuhuri wa hapa nchini, qasida za maombolezo zitakazosomwa na wasomaji qasida wa minasaba ya maombolezo na hotuba fupi itakayotolewa na Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Hassan Khomeini, msimamizi wa haram ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, ni miongoni mwa ratiba za hauli hiyo.
Kutokana hauli ya mwaka huu ya Imam Khomeini (MA) kusadifiana na mwezi mtukufu wa Ramadhani, shughuli hiyo itafanyika wakati wa jioni badala ya asubuhi kama ilivyozoeleka ili kuwafanyia wepesi waombolezaji wanaoshiriki kwenye hauli hiyo.
Kesho Jumapili tarehe 14 Khordad mwaka 1396 hijria shamsia, sawa na tarehe 9 Ramdhani 1438 hijria qamaria inayosadifiana pia na tarehe 4 Juni 2017 miladia unatimia mwaka wa 28 tangu alipofariki dunia Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu Amrehemu), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Hauli ya Imam Khomeini hufanyika kila mwaka kwenye haram yake toharifu kwa kuhudhuriwa na mamilioni ya mahabubu na wapenzi wa kiongozi huyo mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu kutoka kile pembe ya Iran ya Kiislamu na maeneo mbalimbali ya dunia.../