Iran yaendelea kufanya mashauriano kuhusu matukio yaliyojiri katika eneo
(last modified Tue, 06 Jun 2017 04:13:24 GMT )
Jun 06, 2017 04:13 UTC
  • Iran yaendelea kufanya mashauriano kuhusu matukio yaliyojiri katika eneo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Muhammad Javad Zarif, amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na mawaziri wa mambo ya nje wa Kuwait, Qatar, Lebanon, Algeria na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya kuhusiana na matukio yanayoendelea kujiri katika eneo.

Hatua ya Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain na Misri ya kuvunja uhusiano wao na Qatar ni matukio mapya yaliyojiri katika eneo la Mashariki ya Kati. Nchi hizo zimechukua uamuzi huo baada ya kuituhumu Qatar kuwa inaunga mkono ugaidi, inaingilia masuala ya ndani ya nchi za Kiarabu, inatishia usalama wa taifa wa nchi hizo na inatoa hifadhi kwa magaidi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran jana usiku alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Sheikh Sabah Al-Khalid Al-Sabah, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait, Sheikh Muhammad bin Abdurahman Aal Thani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Jebran Basil, Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon, Abdulkadir Mesahel, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria na Federica Mugherini, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, ambapo alijadili na kubadilishana na mawazo na viongozi hao kuhusiana na matukio mapya yanayojiri Mashariki ya Kati.

Waziri wa Mambo ya Nje Muhammad Javad Zarif

Awali Dakta Zarif alifanya mazungumzo na mawaziri wa mambo ya nje wa Iraq, Oman, Uturuki, Tunisia, Malaysia na Indonesia pia kuhusiana na hali ya mambo katika eneo na kuongezeka mivutano kati ya Qatar na baadhi ya nchi nyengine za Kiarabu.

Aidha katika msimamo na radiamali aliyoonyesha kwa hatua ya Saudia na nchi nyengine kadhaa za Kiarabu ya kuvunja uhusiano wao na Qatar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Ulazimishaji na utumiaji nguvu si suluhisho; na mazungumzo, hasa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, ni jambo lenye udharura".

Zarif amesisitizia ulazima wa mazungumzo na maelewano baina ya nchi jirani na kuongeza kuwa: "Majirani watabaki kuwa majirani daima dawamu na haiwezekani kuibadilisha jiografia".../

Tags