Iran yamkosoa Trump kwa kujiondoa makubaliano ya tabianchi
Iran imemkosoa vikali rais wa Marekani kwa kujiondoa katika Makubaliano ya Kimataifa ya Tabianchi .
Makamu wa Kwnaza wa Rais wa Iran Ishaq Jahangiri akizungumza Jumamosi mjini Tehran kwa munasabwa Siku ya Kimataifa ya Mazingira ameongeza kuwa, Marekani imejiondoa katika mkataba huo wakati inaongoza katika uchafuzi wa hewa duniani.
Kauli hiyo ya Jahangiri imekuja baada ya Rais Donald Trump kutangaza Alhamisi iliyopita kuwa Marekani inajiondoa katika Makubaliano ya Kimataifa ya Tabianchi ya Paris.
Jahangiri amesema Trump amedai kuwa anajiondoa katika mkataba huo kwa ajili ya watu wa Marekani lakini anasahau kuwa uchafuvi wa mazingira mbali na kuwaathiri watu wengine duniani pia ni tishio kwa Wamarekani wenyewe.
Makamu wa kwanza wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema kulinda mazingira ni suala lenye umuhimu mkubwa katika karne ya 21. Aidha amesema Iran inachukua hatua za kuhakikisha mazingira yanalindwa kwa kuwashirikisha wananchi.
Makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi yalifikiwa mjini Paris, Ufaransa mwaka 2015 na kutiwa saini na nchi 194 kwa lengo la kuzuia uchafuzi wa mazingira ambao sasa imegeuka na kuwa janga linalohatarisha mustakabali wa sayari ya dunia.