Jahangiri: Iran iko mstari wa mbele kupambana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51191-jahangiri_iran_iko_mstari_wa_mbele_kupambana_na_ugaidi
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugaidi na kwamba, kama si kujitolea kwa serikali na watu wa Syria na washirika wa nchi hiyo, basi hii leo tishio la kundi la Daesh lingeenea katika nchi zote za kanda hii na maeneo mengine ya dunia.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 29, 2019 03:54 UTC
  • Jahangiri: Iran iko mstari wa mbele kupambana na ugaidi

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugaidi na kwamba, kama si kujitolea kwa serikali na watu wa Syria na washirika wa nchi hiyo, basi hii leo tishio la kundi la Daesh lingeenea katika nchi zote za kanda hii na maeneo mengine ya dunia.

Es'haq Jahangiri ambaye yuko mjini Damascus nchini Syria akiongoza ujumbe wa ngazi za juu amesema kuwa kusimama kidete na mapambano ya watu wa Syria na washirika wao dhidi ya ugaidi vimezaa matunda. 

Ameipongeza serikali na watu wa Syria kwa kupata ushindi dhidi ya makundi ya kigaidi na kitakfiri na kusema makundi hayo yataangamizwa na kutokomezwa kikamilifu na mipango na njama za washirika wao zitaambulia patupu. 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Iran itaendelea kuwa bega kwa bega na watu wa Syria katika ujenzi mpya wa nchi hiyo. Amesema mkutano wa 14 wa kiuchumi wa Tehran na Damascus unatoa ujumbe kwamba, Syria imeingia awamu mpya na kwamba kuna udharura wa kufanyika jitihada kubwa za kuijenga upya nchi hiyo. 

Waziri Mkuu wa Syria akizungumza na Makamu wa Rais wa Iran

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Syria Imad Khamis amesema vikao na safari za mara kwa mara za ujumbe wa kisiasa na kiuchumi wa Iran mjini Damascus ni mwanzo wa uhusiano mpana zaidi baina ya mataifa hayo mawili ndugu na marafiki. Ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu kutokana na misaada yake kwa Syria hususan katika mapambano dhidi ya ugaidi na kusisitiza kuwa ushindi uliopatikana katika uwanja huo ni ushindi wa kambi ya muqawama na nchi mbili za Iran na Syria.