Jahangiri: Iran katu haitagonga mwamba
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesisitiza kuwa, Iran katu haitagonga mwamba na kuongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo mkubwa na usio na kifani kwa mtazamo wa mali asili, nguvu kazi na uongozi wenye busara katika kukabiliana na vikwazo."
Ishaq Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran aliyasema hayo Jumamosi na kuongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo mkubwa pia wa kiutamaduni na kistaarabu na uwezo huo ni ngao ya taifa la Iran katika kipindi cha vikwazo."
Jahangiri ameongeza kuwa, kwa mtazamo wa mali asili na hifadhi za madini na chuma, Iran iko katika nchi 10 zinazoongoza duniani na pia kijiografia nchi hii iko katika eneo muhimu sana.
Kauli hiyo imekuja kufuatia uamuzi wa Marekani wa kuiwekea Iran vikwazo baada ya Rais Donald Trump kuchukua uamuzi wa upande mmoja na ulio kinyume cha sheria wa kuindoa nchi yake katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA.
Tarehe sita Agosti Marekani ilitangaza baadhi ya vikwazo viliyo kinyume cha sheria dhidi ya Iran katika sekta ya viwanda vya kuunda magari na dhahabu. Marekani pia imetangaza azma ya kuiwekea Iran vikwazo vya mafuta kuanzia Novemba 4.