"Daesh na makundi mengine ya kitakfiri yameanzishwa na Marekani na Israel"
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i30334-daesh_na_makundi_mengine_ya_kitakfiri_yameanzishwa_na_marekani_na_israel
Naibu Kamanda wa majeshi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kundi la kigaidi la Daesh na makundi mengine ya kitakfiri yameanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na yamekuwa yakitumiwa na tawala hizo kwa ajili ya kufikia malengo yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2017 09:44 UTC

Naibu Kamanda wa majeshi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kundi la kigaidi la Daesh na makundi mengine ya kitakfiri yameanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na yamekuwa yakitumiwa na tawala hizo kwa ajili ya kufikia malengo yao.

Brigedia Jeneral Ahmad Reza Pourdastan amesema hayo leo na kuongeza kuwa, Marekani ni adui wa daima na wa siku zote wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Naibu Kamanda wa majeshi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mashambulio ya kigaidi ya Jumatano iliyopita hapa mjini Tehran yaliyotekelezwa na wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh ni mwenendelezo wa chuki na uhasama wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Brigedia Jenerali Pourdastan amebainisha kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliwaletea walimwengu ujumbe mpya na kwamba Wamarekani hawataki ujumbe huo usikike ulimwenguni.

Maelfu ya Wairani wakisindikiza miili ya mashahidi wa mashambulio ya kigaidi ya Tehran

Naibu Kamanda wa majeshi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema kuwa, vikosi vya Iran daima viko katika kujiimarisha  na kwamba viko tayari kwa ajili ya kukabiliana na vitisho vya usalama.

Amesema, vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimejiandaa kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za kiusalama na kuwaletea wananchi wa taifa hili amani na utulivu.

Ikumbukwe kuwa, watu 17 waliuawa shahidi na 53 kujeruhiwa katika mashambulio mawili tofauti ya kigaidi ya siku ya Jumatano hapa mjini Tehran yaliyolenga jengo la idara la Bunge la Iran na Haram ya Imam Khomeini MA. Kundi la kigaidi la Daesh limetangaza kuwa, wanachama wake ndio waliohusika na mashambulio hayo mawili ya kigaidi mjini Tehran.