Miaka miwili ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Marekani yaendelea kuyakiuka
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i31788-miaka_miwili_ya_makubaliano_ya_nyuklia_ya_jcpoa_marekani_yaendelea_kuyakiuka
Sambamba na kutimu mwaka wa pili tangu Iran na nchi wanachama wa kundi la 5+1 zilipotia saini makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza tena udharura wa Marekani kuheshimu na kutekeleza makubaliano hayo na kusema kuwa, JCPOA ni makubaliano ya kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 15, 2017 01:43 UTC
  • Miaka miwili ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Marekani yaendelea kuyakiuka

Sambamba na kutimu mwaka wa pili tangu Iran na nchi wanachama wa kundi la 5+1 zilipotia saini makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza tena udharura wa Marekani kuheshimu na kutekeleza makubaliano hayo na kusema kuwa, JCPOA ni makubaliano ya kimataifa.

Muhammad Javad Zarif alisema jana baada ya kuwasili mjini New York kwamba, Washington inapaswa kubadili misimamo yake kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kwamba, makubaliano hayo ni matokeo ya mazungumzo ya miaka kadhaa. Amesema inasikitisha kwamba, sera za siasa zisizo sahihi za Marekani zimetengeneza mazingira yanayoizuia Iran kufaidika ipasavyo na makubaliano hayo.

Javad Zarif

Tarehe 14 Julai mwaka 2015 Iran na nchi 6 kubwa wanachama katika kundi la 5+1 zilitia saini makubaliano ya nyuklia kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran baada ya mazungumzo magumu na ya muda mrefu. Makubaliano hayo ambayo yanajulikana kwa kifupi kwa jina la JCPOA, tarehe 20 Julai mwaka huo huo wa 2015 yalipasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuwa hati ya kimataifa. Makubaliano hayo yalianza kutekelezwa rasmi tarehe 16 Julai 2016. Makubaliano hayo ya nyuklia ya Iran yanahesabiwa kuwa makubaliano ya kimataifa baada ya kupasishwa na Umoja wa Mataifa katika azimio nambari 2231 na wala si makubaliano yanayoihusu nchi moja makhsusi. Nchi zote zilizotia saini makubaliano hayo zilichukua jukumu la kuyatekeleza, na nchi yoyote miongoni mwazo haina haki ya kuyakiuka.

Baada ya serikali ya Donald Trump kushika hatamu za uongozi huko Marekani, kulijitokeza mtazamo mpya huko Washington kuhusu makubaliano ya nyuklia ya Iran, na serikali ya Trump ilianza kuyafasiri kuwa ni makubaliano ya pande kadhaa. Japokuwa misimamo ya Trump kuhusu makubaliano hayo imekuwa ikibadilika na kugongana kabla na hata baada ya kuingia Ikulu ya White House, lakini suala na lengo moja limebakia palepale, nalo ni kutaka kudhoofisha makubalino hayo. Kadiri muda ulivyopita, Trump alitupilia mbali misimamo yake ya kutaka kuyachana, kuyafasiri na kutaka kuandikwa upya makubaliano ya JCPOA kutokana na upinzani wa pande nyingine za makubaliano hayo ya nyuklia ya Iran. Hata hivyo kutokana na kuendelea kuweka vikwazo vya aina mbalimbali, ameizuia Iran kufaidika ipasavyo na makubaliano hayo. Katika mkondo huo Baraza la Seneti la Marekani mwezi Juni uliopita liliiwekea Iran vikwazo vipya kwa kile kilichodaiwa ni uungaji mkono wa Iran kwa ugaidi.

Donald Trump

Hivi sasa baada ya kupita miaka miwili tangu makubaliano ya nyuklia ya Iran yatiwe saini, duru mbalimbali zinaelekeza macho yao kwenye misimamo ya serikali ya Donald Trump kuhusu makubaliano hayo. Hadi Jumatatu ijayo, serikali ya Washington itawasilisha ripoti yake katika Kongresi ya nchi hiyo kuhusu utekelezaji wa Iran wa makubaliano ya JCPOA. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marakani Rex Tillarson anawajibika kuwasilisha ripoti katika Kongresi ya nchi hiyo kila baada ya siku 90 kuhusu jinsi Iran inavyotekeleza makubaliano ya JCPOA. Katika ripoti yake ya kwanza kwa Kongresi mwezi Aprili mwaka huu, Tillerson alithibitisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imetekeleza makubaliano hayo lakini akadai kwamba, Tehran inaunga mkono ugaidi! Hii inaonesha kuwa, sera ya serikali ya sasa ya Marekani ni kudhoofisha makubaliano hayo ya nyuklia kwa lengo la kudumisha vikwazo vya vya nchi hiyo dhidi ya Iran licha ya kukiri kwamba, Tehran imetekeleza vipengee vyote vya JCPOA.

Itakumbukwa kuwa, Jumatano iliyopita majenerali 38 wastaafu wa jeshi la Marekani walimwandikia barua Rais Donald Trump wa nchi hiyo wakisisitiza kwamba, hapana shaka kuwa ni makosa kuchana au kutotekeleza makubaliano ya nyuklia na Iran. Wakati huo huo na kwa kuzingatia mitazamo tofauti ya nchi nyingine kuhusu makubaliano hayo, sasa Marekani imebakia peke yake, na harakati za serikali ya Trump katika uwanja huo zinazidi kuidhihirisha Marekani mbele ya walimwengu kuwa ni nchi isiyowajibika wala kuheshimu majukumu yake.

Mogherini na Zarif

Katika uwanja huo, Mkuu wa Sera za Nje za Umoja wa Ulaya, Bi Federica Mogherini, Jumanne iliyopita alisema kuwa, anaheshimu hatua ya Marekani ya kuchunguza makubaliano ya nyuklia ya Iran, lakini amesisitiza kuwa, Umoja wa Ulaya utadumisha ushirikiano wake na Jamhuri ya Kiislamu.