Kharazi: Kudhoofisha muqawama wa Lebanon ni kutumikia maslahi ya Israel
Mkuu wa Baraza la Kiistratejia la Uhusiano wa Kigeni la Iran amesema kuwa kuudhoofisha muqawama wa Lebanon ni kutumikia maslahi ya utawala wa Kizayuni.
Dakta Kamal Kharazi ameashiria kujitolea jeshi, vikosi vya usalama na muqawama wa Lebanon katika kulinda nchi hiyo na watu wake mbele ya ugaidi wa Kizayuni na wa kitakfiri na kuongeza kuwa, hatua ya baadhi ya nchi ya kuzusha madai yasiyo na msingi dhidi ya muqawama wa Lebanon, itamfurahisha adui ghasibu Mzayuni tu. Mkuu wa Baraza la Kiistratejia la Uhusiano wa Kigeni la Iran ameyasema hayo katika mazungumzo na Tamam Salam Waziri Mkuu wa Lebanon huko Beirut mji mkuu wa nchi hiyo.
Kharazi pia amesema kuchaguliwa Rais wa Lebanon ni kadhia ya ndani na akaeleza matumaini aliyonayo kwamba Rais wa nchi iyo atachaguliwa na Walebanon wenyewe kwa wakati muafaka bila ya uingiliaji kutoka nje.
Tamam Salam pia kwa upande wake ameshukuru uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Lebanon na kutaka kuendelezwa uungaji mkono huo na misaada kwa nchi yake.
Waziri Mkuu wa Lebanon na Mkuu wa Baraza la Kiistratejia la Uhusiano wa Kigeni la Iran wamejadili na kubadilishana mawazo pia kuhusu njia za kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Iran na Lebanon, matukio ya eneo khususan kadhia ya Syria na hali ya mambo ya sasa huko Lebanon.