Rouhani: Hakuna anayeweza kuthubutu kulidhuru jeshi la Iran
Rais Hassan Rouhani amesema mihimili mitatu ya serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaviunga mkono kwa dhati vikosi vya jeshi la Iran na kwa msingi huo hakuna anayeweza kulidhuru jeshi hilo wala Iran.
Rouhani aliyasema hayo jana Jumapili katika mkutano na Ali Larijani, Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na Ayatullah Sadeq Amoli Larijani, Mkuu wa vyombo vya mahakama nchini hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, katika hali ya sasa, hakuna yeyote anayeweza kujaribu kuiletea chokochoko Iran kutokana na namna mihimili yote ya serikali pamoja na Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran zinafanya kazi kwa ushirikiano na kuviunga mkono vikosi vya jeshi la Iran kama vile Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), vikosi vya kujitolea vya wananchi (Basij) na vinginevyo. Rais wa Iran amesema kwa uwezo wa Allah taasisi hizo za serikali zitaendelea kuwa katika mkondo huo.
Kuhusu hatua ya hivi karibuni ya Kongresi ya Marekani ya kupasisha vikwazo vipya dhidi ya Iran, Rais Rouhani amesema iwapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itazidi kuimarisha ushirikiano wake wa kiuchumi na nchi nyingine za dunia, basi Washington haitaendelea kutumia silaha iliyofeli ya vikwazo dhidi ya Tehran.
Dakta Rouhani amesema kwa sasa mambo muhimu yanayoishughulisha Iran ni kuongeza uzalishaji, kupanua nafasi za ajira na kuimarisha uchumi.
Wizara ya Fedha ya Marekani imeyaweka mashirika sita ya Iran katika orodha yake ya vikwazo kama radiamali ya kukabiliana na hatua ya Iran ya kufanyia kwa mafanikio majaribio ya roketi la kubeba satalaiti la Simorgh hapa nchini.
Siku ya Jumamosi, Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alivizungumzia vikwazo hivyo vya US dhidi ya Iran akisema kuwa, Tehran haitasita kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama JCPOA, iwapo 'madhara yatapiku faida'.