Rais Rouhani: Iran iko tayari kustawisha uhusiano na nchi za Afrika
Rais Hassan Rouhani amesema mabara mawili ya Asia na Afrika yana maslahi mengi ya pamoja kwa ajili ya kushirikiana na kuongeza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalipa umuhimu mkubwa suala la kustawisha uhusiano na nchi za Afrika.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Swaziland, Barnabas Sibusiso Dlamini na kuongeza kuwa Tehran iko tayari kustawisha uhusiano na ushirikiano na nchi zote za Afrika ikiwemo Swaziland.
Dakta Rouhani amesema ugaidi umevuruga amani katika sehemu kadhaa za bara la Afrika na kufafanua kwamba moja ya majukumu makubwa uliyonayo ulimwengu wa leo ni kuleta amani na uthabiti katika nchi mbalimbali duniani na kupambana na visababishi vya ukosefu wa amani na uthabiti hususan ugaidi.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Swaziland Barnabas Sibusiso Dlaminia amesema nchi yake inakupa umuhimu wa aina yake kuimarisha uhusiano wake na Iran na imedhamiria kuzidisha ushirikiano wake na Jamhuri ya Kiislamu katika nyanja tofauti.
Rais Rouhani amefanya mazungumzo pia na Mfalme Letsie III wa Lesotho ambapo amesisitizia tena umuhimu ambao Iran imekuwa inalipa siku zote suala la kustawisha uhusiano wa kirafiki na nchi za Afrika na kuongeza kwamba ana matumaini safari ya Mfalme wa Lesotho hapa Tehran utakuwa mwanzo wa kustawishwa ushirikiano na uhusiano wa Iran na nchi hiyo.
Kwa upande wake, Mfalme Letsie III wa Lesotho amesema nchi yake inaheshimu na kutilia mkazo kuishi kwa masikilizano, kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine pamoja na kuleta utulivu, amani na usalama na akataka kustawishwa uhusiano na ushirikiano kati ya nchi yake na Iran.../