Balozi wa Iran UN: Marekani ijifunze kutokana na makosa iliyofanya huko nyuma
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i33328-balozi_wa_iran_un_marekani_ijifunze_kutokana_na_makosa_iliyofanya_huko_nyuma
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikipigania amani na uthabiti; na amewataka viongozi wa Marekani wajifunze kutokana na makosa waliyofanya huko nyuma.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 18, 2017 22:40 UTC
  • Balozi wa Iran UN: Marekani ijifunze kutokana na makosa iliyofanya huko nyuma

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikipigania amani na uthabiti; na amewataka viongozi wa Marekani wajifunze kutokana na makosa waliyofanya huko nyuma.

Gholamali Khoshroo ameyasema hayo kujibu madai ya kichochezi yaliyotolewa hivi karibuni dhidi ya Iran na Nikki Haley, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa taarifa ya Agosti 15 iliyotolewa na Haley haina lolote la ukweli ndani yake.

Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika UN ameongeza kuwa matamshi makali na tuhuma zisizo na msingi zilizotolewa hivi karibuni na Nikki Haley dhidi ya Iran ni mfano mmojawapo wa hatua za kichochezi, vitisho vya wazi na hatua zisizo na nadhari za viongozi wa Marekani za kutaka kuchafua sura ya Iran na kudhoofisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, jambo ambalo linakinzana na ahadi ambazo Marekani imetoa katika makubaliano hayo.

Siku ya Jumanne iliyopita, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa alidai kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaswa kuwajibika kwa hatua zake za "kurusha makombora, kuunga mkono ugaidi na kukiuka maazimio ya Baraza la Usalama". 

Nikki Haley

Khoshroo amesisitiza kuwa mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa anapaswa kujifunza kutokana na historia na kuwafunza pia baadhi ya viongozi wengine wa nchi hiyo ili wasirudie makosa yaleyale waliyofanya huko nyuma.

Kinyume na misimamo ya pande nyingine husika katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, yaani Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Russia, China pamoja na Umoja wa Ulaya, Washington imekuwa ikifanya kila njia za kukwamisha utekelezaji wa makubaliano hayo.

Marekani inadai kuwa majaribio ya makombora yanayofanywa na Iran yanakiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwamba majaribio hayo yanajumuisha makombora yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia, ilhali  Nabila Massrali, msemaji wa Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya alitangaza hivi karibuni kuwa majaribio ya makombora ya Iran hayakiuki makubaliano ya JCPOA.../