Bunge laidhinisha uteuzi wa mawaziri 16 waliopendekezwa na Rais Rouhani
Wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran wamewapigia kura ya kuwa na imani nao mawaziri 16 kati ya 17 waliopendekezwa na Rais Hassan Rouhani kuunda baraza la mawaziri la serikali yake mpya, baada ya vikao vya siku nane vya kuchunguza sifa za mawaziri hao.
Abbas Akhundi, amepitishwa kwa kura 188 kuwa Waziri wa Barabara na Ujenzi wa Miji, Masoud Soltani amekuwa Waziri wa Michezo na Vijana baada ya kupitishwa kwa kura 225, Abdoreza Rahmani Fazli amepigiwa kura 250 za kuwa na imani naye ili kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani, Mohammad Javad Zarif ataongoza tena Wizara ya Mambo ya Nje baada ya kupitishwa kwa kura 236 na Bijan Namdar Zanganeh amepata kura 230 za kuwa na imani naye na kumwezesha kuongoza tena Wizara ya Mafuta.
Wabunge wa Bunge la Iran aidha wamepiga kura 244 za 'ndiyo' kumpitisha Ali Reza Avaei kuongoza Wizara ya Sheria, kura 240 kumpitisha Masoud Karbasiyan kuongoza Wizara ya Uchumi na Fedha, kura 242 kumpitisha Sayyed Abbas Salehi kuongoza Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu na kura 241 kumpitisha Mohammad Shariatmadari kuongoza Wizara ya Viwanda, Madini na Biashara.
Sayyid Mahmoud Alavi amepata kura 252 kumwezesha kuongoza Wizara ya Usalama, Ali Rabei amepata kura 191 za kumuidhinisha kuongoza Wizara ya Ushirika, Kazi na Ustawi wa Jamii na Brigedia Jenerali Amir Hatami amepitishwa kuwa Waziri wa Ulinzi kwa kura 261.
Bunge la Iran limempigia kura 164 za kuwa na imani naye Mahmoud Hojjati kuongoza Wizara ya Jihadi ya Kilimo, kura 152 Mohammad Azar Jahromi kuongoza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kura 253 Sayyed Hassan Qazi Hashemi kuongoza Wizara ya Afya na Tiba. Mohammad Bat-hai amepata kura 238 za kuwa na imani naye na kupitishwa kuwa Waziri wa Elimu na Malezi.
Hata hivyo Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran haikumpigia kura za kuwa na imani naye Habibollah Bitaraf aliyependekezwa na Rais Rouhani kuongoza Wizara ya Nishati.
Katika upigaji kura, Bitaraf alipata kura 133 za 'ndiyo', 132 za 'hapana', wabunge 17 hawakupiga kura na kura nyengine 6 ziliharibika.
Jumla ya wabunge 279 walihudhuria kikao cha leo cha kuwapigia kura mawaziri wapendekezwa.../