IAEA: Iran imetekeleza majukumu yake yote kuhusu JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i33841-iaea_iran_imetekeleza_majukumu_yake_yote_kuhusu_jcpoa
Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) umetoa ripoti yake ya msimu ukisisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza majukumu yake yote kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 31, 2017 22:58 UTC
  • IAEA: Iran imetekeleza majukumu yake yote kuhusu JCPOA

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) umetoa ripoti yake ya msimu ukisisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza majukumu yake yote kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Ripoti mpya ya msimu ya wakala wa IAEA kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran ilitolewa jana na kukabidhiwa kwa wanachama wote wa Baraza la Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia. 

Katika ripoti hiyo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia umethibitisha tena kwamba, Iran imeheshimu na kutekeleza majukumu yake.

Hiyo ni ripoti ya 8 ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia, Bwana Yukia Amano tangu tarehe 16 Januari mwaka jana yalipoanza kutekelezwa makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi wanachama wa kundi la 5+1. 

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kundi la 5+1, Vienna

Makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 kwa kifupi JCPOA yalitiwa saini tarehe 14 Julai mwaka 2015 mjini Vienna, Austria baada ya mazungumzo magumu na ya muda mrefu. 

Ni vyema kuashiria hapa kwamba ripoti zote 8 zilizotolewa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia zimesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza kikamilifu majukumu yake kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.