Yukiya Amano: Iran inatekeleza ahadi zake kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kwa mara nyingine tena amethibitisha kwamba, Iran imeheshimu na kufungamana na ahadi zake zote kuhusiana na makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Yukiya Amano amesema hayo leo mwanzoni mwa kikao cha msimu cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki huko Vienna, Austria na kueleza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeheshimu na kufungamana kikamilifu na ahadi zake katika makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa na kutiwa saini mwaka 2015 kati yake na kundi la 5+1 linaloundwa na nchi za Marekani, Ufaransa, Uingereza, China, Russia pamoja na Ujerumani.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomikia (IAEA) amebainisha kwamba, masharti ambayo Iran iliyakubali yamo katika hatua ya utekelezwaji.
Uthibitisho huo wa Yukiya Amano wa kufungamana Iran na ahadi zake kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA unatolewa katika hali ambayo, ikulu ya Marekani White House imedai kwamba, Iran haijafungamana na makubaliano ya nyuklia na imo katika kuchukua hatua za kuishinikiza Jamhuri ya Kiislamu.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, hadi sasa serikali ya Marekani imeshindwa kutoa ushahidi wa madai yake kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijafungamana na makubaliano ya nyuklia. Ikumbukwe kuwa pia, ripoti ya nane ya msimu ya IAEA iliyotolewa tarehe 31 ya mwezi uliopita wa Agosti iliunga mkono na kuthibitisha kwamba, Iran imefungamana na ahadi zote zote kuhusiana na makubaliano ya nyuklia. Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Marekani na Rais Donald Trump wa nchi hiyo wamekuwa kila mara wakichukua hatua za kukwamisha utekelezwaji wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.