Rais Rouhani wa Iran aelekea New York katika mkutano wa UN
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i34471-rais_rouhani_wa_iran_aelekea_new_york_katika_mkutano_wa_un
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ni kwa maslahi ya amani na uthabiti sio tu kwa eneo hili la Mashariki ya Kati bali kwa dunia nzima.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 17, 2017 03:21 UTC
  • Rais Rouhani wa Iran aelekea New York katika mkutano wa UN

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ni kwa maslahi ya amani na uthabiti sio tu kwa eneo hili la Mashariki ya Kati bali kwa dunia nzima.

Rais Rouhani ameyasema hayo mapema leo Jumapili hapa mjini Tehran, kabla ya kuondoka kuelekea mjini New York kwenda kushiriki duru ya 72 ya Mkutano wa Kawaida wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA.

Amesema hakuna shaka kwamba hii leo kuna kauli na msimamo mmoja kuwa makubaliano hayo yana manufaa katika uwanja wa usalama, uthabiti na maendeleo kieneo na kimataifa. Hata hivyo amesisitiza kuwa, ni nchi chache tu kama Marekani zinazopinga makubaliano hayo ya JCPOA na zinahisi kuwa 'zilihadaiwa'.

Rais wa Iran amesema Iran itatumia jukwaa la mkutano huo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuifahamisha dunia kuhusu manufaa ya JCPOA sambamba na kuondoa kasumba na propaganda zinazoenezwa na Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi kuhusu makubaliano hayo ya kihistoria.

Rais Rouhani katika mkutano wa nyuma wa UNGA

Dakta Rouhani amesema anatazamia kukutana na kufanya mazungumzo na Marais wa Ubelgiji, Austria, Ufaransa, Japan, Pakistan, Afrika Kusini na Bolivia miongoni mwa wengine, kujadili nukta kadhaa, kukiwemo kuimarishwa uhusiano wa pande mbili, fursa za kustafidi na makubaliano ya nyuklia ya Vienna, pamoja na mgogoro unaondelea hivi sasa wa Myanmar. 

Kadhalika Rais wa Iran amesema jinamizi la ugaidi ni suala jingine litakalopewa kipaumbele katika mkutano wake na marais na wakuu wengine wa nchi, pambizoni mwa mkutano wa UN.