Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu kuhusu uafiriti wa Marekani juu ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i34507-mtazamo_wa_kiongozi_muadhamu_kuhusu_uafiriti_wa_marekani_juu_ya_jcpoa
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran amezungumzia uafiriti na ukhabithi wa Marekani kuhusu makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina maarufu la JCPOA na kusisitiza kuwa, kosa lolote litakalofanywa kuhusu makubaliano hayo litapata majibu kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 18, 2017 01:40 UTC
  • Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
    Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran amezungumzia uafiriti na ukhabithi wa Marekani kuhusu makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina maarufu la JCPOA na kusisitiza kuwa, kosa lolote litakalofanywa kuhusu makubaliano hayo litapata majibu kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema hayo jana katika sherehe za kuhitimu mafunzo wanachuo wa Chuo Kikuu cha Jeshi la Polisi na kubainisha kwamba, wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais nchini Marekani mwaka 2016, Donald Trump alishikilia kwamba hayapendi makubaliano ya JCPOA na kuahidi kuyachana iwapo atachaguliwa. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameonya kwa kusema: Iwapo Wamarekani watayachana makubaliano ya JCPOA, basi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itayachoma moto kabisa makubaliano hayo.

Amirijeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Iran akikagua gwaride

 

Ayatullah Khamenei aidha ameashiria namna Wamarekani wasivyo na mwamana hata kidogo katika vitendo na ahadi zao na kubainisha kuwa, katika suala hili la JCPOA, kila leo utawaona Wamarekani wanafanya uafiriti mpya na huo ni uthibitisho wa ukweli wa maneno ya Imam Khomeini MA aliposema, Marekani ni shetani mkubwa, na kwa hakika utawala wa Marekani ni shetani khabithi na afiriti zaidi duniani.

Makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina la JCPOA ni makubaliano yaliyofikiwa baina ya Iran na nchi kubwa sita za dunia. Hata hivyo tangu yalipoanza kutekelezwa mwezi Januari 2016, kila leo Marekani inayavunja waziwazi makubaliano hayo. Hatua zote zilizochukuliwa na Marekani katika kipindi hiki cha miezi 20 ya utekelezaji wa JCPOA zimelenga kuyavunja makubaliano hayo. Marekani inatenda kinyume kabisa na ahadi zake za wakati wa mazungumzo yaliyofanikisha makubaliano hayo. Hata hivyo, kabla ya jambo lolote, uvunjaji huo wa ahadi unaofanywa na Wamarekani umezidi kulithibitishia taifa la Iran kwamba Marekani ni dola la kibeberu lisilo na mwamana hata chembe na kamwe haliwezi kuachana na uadui wake dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Sehemu ya sherehe za kumaliza masomo wanachuo wa Chuo Kikuu cha Jeshi la Polisi nchini Iran. Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu akikagua gwaride.

 

Miongoni mwa uvunjaji huo wa wazi wazi wa JCPOA ni kitendo cha Marekani cha kuweka vikwazo vipya dhidi ya Jamnuri ya Kiislamu ya Iran. Lakini kama ambavyo taifa na viongozi wa Iran wamesimama kidete katika kipindi cha miongo minne iliyopita, ni vivyo hivyo wataendelea kusimama imara kukabiliana na uafiriti wa Marekani katika makubaliano haya ya nyuklia. Kuhusu ukhabithi unaofanywa na Marekani wa kukwamisha utekelezaji wa makubaliano ya JCPOA, taifa la Iran haliwezi kamwe kuruhusu uafiriti huo ukanyage haki za taifa hili la Kiislamu. Katika kipindi cha baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, taifa hili limethibitisha kivitendo kuwa si la watu wanaokubali kuburuzwa na madola ya kibeberu. Akizungumzia uhakika huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema jana kuwa, Wamarekani wanapaswa kutambua vyema kwamba, taifa la Iran litaendelea kuwa imara katika kulinda misimamo yake kwa heshima na kwa nguvu zote na kamwe halitorudi nyuma. Aidha Wamarekani wanapaswa kuelewa vyema kuwa, kurudi nyuma ni msamiati ambao haumo kabisa katika kamusi ya Jamhuri ya Kiislamu na hautakuwemo kamwe.

Ukweli wa mambo ni kuwa, uafiriti na chokochoko za hivi sasa za Marekani kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA haziwezi kamwe kuathiri misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tehran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa itasimama imara kulinda makubaliano hayo ya nyuklia, lakini wakati huo huo imeonya kwamba, haiwezi kukubaliana na ubeberu wa Marekani. Kamwe Iran haitaruhusu Wamarekani watumie makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kupata siri za Jamhuri ya Kiislamu au kukagua vituo vya kijeshi vya Iran na wanaihesabu fikra hiyo ya Marekani kuwa ni ndoto za alinacha tu.