Machaguo ya Iran mkabala na kujiondoa Trump katika makubaliano ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i34649-machaguo_ya_iran_mkabala_na_kujiondoa_trump_katika_makubaliano_ya_jcpoa
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mazingira mapya yataandaliwa na kwamba Iran inayo haki ya kuwa na chaguo lake iwapo Marekani itajiondoa katika makubaliano ya JCPOA. Rais Rouhani ameyatamka hayo alipozungumza na televisheni ya NBC ya Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 21, 2017 03:04 UTC
  • Machaguo ya Iran mkabala na kujiondoa Trump katika makubaliano ya JCPOA

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mazingira mapya yataandaliwa na kwamba Iran inayo haki ya kuwa na chaguo lake iwapo Marekani itajiondoa katika makubaliano ya JCPOA. Rais Rouhani ameyatamka hayo alipozungumza na televisheni ya NBC ya Marekani.

Akibainisha namna wanachama wengine wa kundi la 5 +1 wanavyotilia mkazo kuheshimiwa makubaliano ya JCPOA, Dakta Rouhani ameeleza kuwa, JCPOA ni makubaliano yaliyofikiwa na nchi saba na kuidhinishwa na Umoja wa Mataifa; na ahadi za Iran katika hali mpya ya mambo hazitakuwa kama huko nyuma iwapo moja ya nchi hizo itakengeuka makubaliano hayo. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza mara kadhaa kwamba Iran kamwe haitakiuka makubaliano ya JCPOA, lakini  haitakaa kimya  mkabala na kuvurugwa makubaliano hayo na kwamba inayo machaguo tofauti kuhusiana na suala hilo.

wawakilishi wa nchi zilizotia saini mapatano ya JCPOA

Hatua ya kwanza na ya haraka itakayochukuliwa na Iran katika kukabiliana na ukiukaji wowote wa makubaliano ya JCPOA ni kurejea katika shughuli zake za nyuklia za huko nyuma. Iwapo Rais Donald Trump wa Marekani atajiondoa kwenye makubaliano hayo, basi shughuli za sentrifuji hapa Iran zitakuwa kama ilivyokuwa huko nyuma kabla ya mazungumzo ya nyuklia. 

Siasa  za serikali zilizotangulia za Marekani zilipelekea idadi ya sentrifuji hapa nchini kufikia mashine karibu elfu 20 kutoka karibu 200; na leo hii si kazi ngumu kwa Iran kukariri hali hiyo na kuzungusha sentrifuji zote hizo. Aidha uzoefu umethibitisha kuwa Iran huchukua maamuzi magumu kulingana na hali ya mambo mkabala na machaguo yake. Karibu miaka arubaini iliyopita wananchi wa Iran wamethibitisha kutosalimu amri mbele ya madai na matamshi yasiyo na msingi ya viongozi wa Marekani na kamwe hawatatumbukia katika mtego huo.

Trump, Rais mwenye kiburi wa Marekani

Matamshi ya kijahili yaliyotolewa na Trump siku ya Jumanne katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kamwe hayawezi kuwa msingi wa maamuzi yanayochukuliwa na nchi nyingine kuhusu JCPOA; bali matamshi hayo yamedhihirisha namna rais huyo wa Marekani asivyo na taarifa na ufahamu wa kutosha kuhusu sheria na maazimio ya kimataifa na jinsi alivyotekwa na ukandamizaji wa wengine akiwemo Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni. Netanyahu anataka Marekani ijiondoe katika mapatano ya JCPOA au yafanyike mazungumzo mapya ili kuyafanyia marekebisho makubaliano hayo; ndoto ambayo kamwe haiwezi kutumia. 

Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni