Maadhimisho ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu Iran yaanza kwa hotuba ya Rouhani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i34699-maadhimisho_ya_wiki_ya_kujihami_kutakatifu_iran_yaanza_kwa_hotuba_ya_rouhani
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema hakuna chochote kinachoweza kuizuia Jamhuri ya Kiislamu kuendelea kuimarisha uwezo wake wa makombora na mifumo ya kiulinzi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 22, 2017 04:40 UTC
  • Maadhimisho ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu Iran yaanza kwa hotuba ya Rouhani

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema hakuna chochote kinachoweza kuizuia Jamhuri ya Kiislamu kuendelea kuimarisha uwezo wake wa makombora na mifumo ya kiulinzi.

Rais Rouhani ameyasema hayo leo Ijumaa katika hotuba yake aliyoitoa kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Kujihami Kutakatifu na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kujiimarisha kijeshi namna inavyotaka.

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, uwezo mkubwa wa kijeshi wa nchi hii haujawahi kutumiwa katika kuzivamia nchi nyingine, katika hali ambayo madola ya kibeberu yanamwaga silaha za maangamizi katika eneo hili la Mashariki ya Kati ili kuvuruga amani na uthabiti.

Wanajeshi wa Iran wakipita mbele ya Rais Rouhani

Amebainisha kuwa: "Taifa lenye izza la Iran daima limekuwa katika njia ya kutafuta amani na usalama sio tu katika eneo bali kote duniani na litaendelea kutoa uungaji mkono na kuwapa himaya wananchi madhulumu na wanaonyongeshwa katika nchi kama vile Yemen, Syria na Palestine, wapende wasipende."  

Maadhimisho ya miaka 36 ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu nchini yameanza kwa mbwembwe ya aina yake, ambapo mapema leo asubuhi vikosi tofauti vya Jeshi la Iran vimepiga magwaride hapa jijini Tehran na katika miji mingine.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huadhimisha Wiki ya Kujihami Kutakatifu kila mwaka kama kumbukizi ya vita vya miaka minane vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran mwaka 1980-1988.

Moja ya vikosi vya Jeshi la Iran