Ayatullah Amoli Larijani: Utawala wa Kizayuni unatekeleza siasa za kuigawa Iraq
Mkuu wa Chombo cha Mahakama nchini Iran amesema kuwa kufanyika kura ya maoni ya kujitenga eneo la Kurdistan huko Iraq ni njama moja inayotekelezwa na madola ya kiistikbari khususan utawala wa Kizayuni ili kulishughulisha eneo hili.
Ayatullah Sadeq Amoli Larijani amesema kuwa siasa za kuzigawa nchi za Kiislamu ni siasa zinazoendeshwa na utawala wa Kizayuni lengo likiwa ni kuzidhoofisha serikali za Kiislamu na kuzusha mapigano ya muda mrefu katika mataifa ya Kiislamu; siasa ambazo kwa bahati mbaya zimeliathiri pia eneo la Kurdistan ya Iraq. Ayatullah Larijani ameyasema hayo leo hapa Tehran katika kikao na maafisa wa ngazi za juu wa chombo cha mahakama.
Mkuu wa Chombo cha Mahakama hapa nchini amesema kuwa siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinapinga hatua yoyote yenye lengo la kuleta mgawanyiko na kwamba viongozi husika wa eneo la Kurdistan huko Iraq hawatafanikiwa katika suala hilo la kutaka kujitenga eneo hilo.
Ayatullah Amoli Larijani ameeleza kufurahishwa na hali ya muqawama katika eneo hilo na ushindi mtawalia wa harakati hiyo na kueleza kuwa, kundi la kigaidi la Daesh na mirengo ya kitakfiri imefikia ukingoni. Amesema, makundi hayo hivi sasa yanaangamizwa kutokana na juhudi za wananchi na vikosi vya Syria na Iraq na pia uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.