Kuimarishwa uhusiano wa Iran na Umoja wa Afrika
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Umoja wa Afrika, AU katika sekta za sayansi, teknolojia, kilimo, kijamii na uchumi.
Hayo yamebainika Jumatatu wakati Balozi Mehdi Agha Jaafari Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika Katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alipotembelea makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia na kufanya mazungumzo na wakuu wa umoja huo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Irna, Agha Jaafari alikutana na maafisa wa ngazi za juu wa AU na pia wawakilishi wa tume za sayansi na teknolojia, kijamii, kilimo na kiuchumi katika umoja huo. Mazungumzo hayo yalihusu njia za kuimarisha ushirikiano wa Iran na Umoja wa Afrika katika nyuga mbali mbali.

Katika kikao hicho, wakuu wa Umoja wa Afrika walikaribisha kuendelezwa ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku wakisisitiza kuimarishwa uhusiano wa pande mbili.
Mwaka jana wawakilishi wa tume za Umoja wa Afrika za sayansi na teknolojia, kijamii, kilimo na kiuchumi walitembelea Iran ambapo kulitiwa saini mapatano ya ushirikiano na idara husika nchini Iran.
Kabla ya kutembelea makao maku ya AU, Balozi Mehdi Agha Jaafari alitangulia kuzitembelea Uganda na Burundi na kukutana na wakuu wa nchi hizo hizo kuhusu kuimarishwa uhusiano na Iran. Akiwa nchini Ethiopia pia amekutana na kufanya mazungumzo na waziri wa mafuta na madini wa nchi hiyo na maafisa wengine wa ngazi za juu. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalipatia kipaumbele suala la kuimarisha uhusiano wa kiuchumi,kisisa na kiutamaduni na nchi za bara Afrika.