Oct 16, 2017 12:04 UTC
  • Larijani: Ugaidi ni hatari kwa dunia nzima

Spika wa majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, ugaidi ni hatari kubwa kwa usalama wa nchi zote duniani na mapambano dhidi ya uhalifu huo mkubwa yanahitajia ushirikiano wa nchi zote duniani.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu Ali Larijani akisema hayo leo pambizoni mwa kikao cha 137 cha Umoja baina ya Mabunge ya Dunia kinachoendelea mjini Saint Petersburg, Russia. Dk Larijani amesema hayo katika mazungumzo yake na Bukola Saraki, Spika wa Baraza la Senate la Nigeria na kuongeza kuwa, Iran na Nigeria zinaweza kushirikiana vizuri katika nyuga tofauti hususan uwanja wa mafuta na gesi.

Spika wa Bunge la Iran katika mkutano wa Saint Petersburg nchini Russia

 

Kwa upande wake, Bukola Saraki, Spika wa Bunge la Nigeria amesisitiza kuwa, Iran hivi sasa iko katika mstari wa mbele wa kupambana na ugaidi na inabidi nchi nyingine duniani ziige mfano wa Iran wa kupambana vilivyo na hatari hiyo kubwa ya ugaidi duniani.

Spika wa bunge la Nigeria ameongeza kuwa, nchi yake inataka kuimarisha uhusiano wake na Iran katika nyuga zote hasa za uchumi na bunge.

Spika wa Bunge la Iran yuko mjini Saint Petersburg, Russia hivi sasa na huko ameonana na maspika wa mabunge ya Syria, Oman, Kuwait, Uturuki, Iraq, Mexico, Armenia pamoja na katibu mtendai wa Taasisi ya Kuzuia Majaribio ya Nyuklia CTBT na amejadiliana nao masuala mengi ya pande mbili, ya kieneo na ya kimataifa.

Tags