Ayatullah Shirazi: Waislamu wasinyamazie kimya jinai dhidi ya wenzao wa Rohingya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i36030-ayatullah_shirazi_waislamu_wasinyamazie_kimya_jinai_dhidi_ya_wenzao_wa_rohingya
Ayatullah Makarim Shirazi ambaye ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Kiislamu nchini Iran ameeleza kusikitishwa kwake na hali mbaya inayozidi kuwakabili Waislamu wa jamii ya Rohingya huku akiwataka Waislamu kote duniani kutofumbia macho jinai wazofanyia ndugu zao nchini Myanmar.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 29, 2017 12:32 UTC
  • Ayatullah Shirazi: Waislamu wasinyamazie kimya jinai dhidi ya wenzao wa Rohingya

Ayatullah Makarim Shirazi ambaye ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Kiislamu nchini Iran ameeleza kusikitishwa kwake na hali mbaya inayozidi kuwakabili Waislamu wa jamii ya Rohingya huku akiwataka Waislamu kote duniani kutofumbia macho jinai wazofanyia ndugu zao nchini Myanmar.

Ayatullah Naser Makarem Shirazi mmoja wa Marjaa Taklidi wa Qum nchini Iran ameyasema hayo leo Jumapili katika mji wa Qum, wakati wa kikao na maafisa wa Shirika la Hilali Nyekundu la Iran na kusisitiza kuwa, Waislamu wa Rohingya wanakabiliwa na hali mbaya ya kutisha katika nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia.

Kadhalika amesema Waislamu hao wa Rohingya wanakabiliwa na hali ngumu ya kibinadamu sio ndani ya Myanmar wanakouawa na kukandamizwa kila uchao, bali pia nchini Bangladesh walikokimbilia usalama wao.

Mbali na kuuawa, wanawake Waislamu wa Rohingya wamekuwa wakinajisiwa na kubakwa

 

Mwanachuoni huyo mashuhuri wa Iran amebainisha kuwa: "Sisi kama Waislamu, hatuna budi kushikana mikono na kuhakikisha kuwa tunawasadia ndugu zetu wa Rohingya. Hilo ni jukumu letu la kidini kwa kuwa Waislamu wote ni ndugu."

Malefu ya Waislamu Rohingya wameuawa na malaki ya wengine wamelazimishwa kuwa wakimbizi katika nchi jirani ya Bangladesh tangu tarehe 25 mwezi Agosti mwaka huu, kutokana na mauaji yanayofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali wakishirikiana na jeshi la serikali ya Myanmar katika mkoa wa Rakhine.