Iran itashiriki vilivyo katika kuijenga upya Syria
Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran itashiriki vilivyo katika utekelezaji wa mipango itakayoainishwa na serikali ya Syria katika kujenga upya sekta mbali za uzalishaji, utoaji huduma na ustawi zilizoharibiwa vibaya na magenge ya kigaidi yaliyoivamia nchi hiyo ya Kiarabu.
Shirika la habari la IRIB limemnukuu Bw. Mohammad Shariatmadari akisema hayo jana wakati alipoonana na Bw. Adnan Mahmoud, balozi wa Syria hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, sekta binafsi za nchi hizo mbili zinapaswa kushirikiana vilivyo na sekta za serikali katika kufanikisha miradi mikubwa ya kiuchumi na kutumia vyema uwezo uliopo katika nchi hizi.
Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara ya Iran amesema kuwa nchi yake iko tayari wakati wote kuimarisha ushirikiano wake wa kiuchumi na Syria katika kiwango cha kiistratijia na kuongeza kuwa, kwa uwezo wa Allah, Tehran itairejesha katika hali ya kawaida sekta ya viwanda ya Syria.
Aidha amesema, serikali ya Iran itaendelea pia kuisaidia Syria katika juhudi zake za kurejesha amani na utulivu nchini humo.
Kwa upande wake, Adnan Mahmoud, balozi wa Syria nchini Iran amesema, hatua za lazima zimeshachukuliwa kwa ajili ya kutekeleza kivitendo hati ya maelewano iliyotiwa saini baina ya nchi hizi mbili kwa ajili ya kuendesha miradi ya viwanda, kutenga maeneo maalumu ya viwanda na kufunguliwa matawi ya benki katika nchi mbili za Iran na Syria kwa ajili ya kurahisisha na kupandisha juu kiwango cha mabadilishano ya kibiashara baina ya nchi hizi mbili.