Rais Putin wa Russia atarajiwa Iran kuhudhuria mkutano wa pande tatu
Rais Vladimir Putin wa Russia na Rais Ilham Aliyev wa Jamhuri ya Azerbaijan leo Jumatano wanatarajiwa kuwasili mjini Tehran kwa ajili ya mkutano wa pande tatu na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mkutano huo wa pande tatu utakuwa ni wa pili wa pande hizo tatu baada ya ule ambao uliofanyika Agosti mwaka jana katika Jamhuri ya Azerbaijan na kuhudhuriwa na marais hao watatu.
Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi, viongozi hao wawili wataandamana na jumbe za ngazi za juu katika nyanja mbali mbali hasa za kisiasa na kiuchumi.
Viongozi wa nchi hizo tatu watajadili masuala muhimuu ya uhusiano baina ya nchi zao, kieneo na kimataifa.
Qassemi ameongeza kuwa, kumeshafanyika mipango maalumu ya mkutano wa pamoja wa marais Putin wa Russia na Aliyev wa Jamhuri ya Azebaijan na mwenzao wa Iran. Nchi hizo mbili zinapakana na Iran na mkutano huo unatathminiwa kuwa ni wenye umuhimu mkubwa kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa.