Mar 23, 2016 07:21 UTC
  • Iran yalaani mashambulizi ya kigaidi ya Brussels

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea jana katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels na kusababisha vifo vya makumi ya watu.

Hussein Jaberi Ansari ametuma salama za rambirambi kwa familia za wahanga wa hujuma hiyo ya kigaidi, serikali na taifa hilo kwa jumla. Katika ujumbe wake, Jaberi Ansari amesema wimbi la mashambulizi ya kigaidi katika maeneo mbalimbali ya dunia linaashiria kuwa ugaidi ni jinamizi linalokodolea macho dunia nzima na kusisitiza kuwa, kuna haja kwa nchi zote za dunia kushirikiana ili kulishinda jinamizi hilo.

Awali Rais Hassan Rouhani wa Iran na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu Muhammad Javad Zarif walilaani mashambulizi hayo ya jana. Kadhalika Taasisi na jumuiya mbalimbali za Kiislamu zimelaani vikali mashambulizi hayo ya kigaidi yaliyolenga uwanja wa ndege na kituo cha treni ya chini kwa chini mjini Brussels na kusema kuwa, mashambulizi hayo yamefanywa na wahalifu na wauaji wasio na chembe ya huruma.

Miripuko ya kigaidi ilitokea asubuhi ya jana mjini Brussels katika uwanja wa ndege na treni ya kasi ya chini ya ardhi (metro) na kuua watu wasiopungua 34 huki zaidi ya 190 wakijeruhiwa. Kundi la kigaidi na kitaifiri la Daesh limekiri kuhusika na mashambulizi hayo ya kikatili.

Tags