'Iran ni nchi pekee inayounga mkono ukombozi wa taifa la Palestina'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i36310-'iran_ni_nchi_pekee_inayounga_mkono_ukombozi_wa_taifa_la_palestina'
Msemaji wa Baraza la Maulamaa wa Palestina nchini Lebanon amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo nchi pekee inayounga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina na kwamba baraza hilo liko tayari kuungana na nchi zote za Kiarabu na Kiislamu kwa ajili ya ukombozi wa Palestina:
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 10, 2017 23:43 UTC
  • 'Iran ni nchi pekee inayounga mkono ukombozi wa taifa la Palestina'

Msemaji wa Baraza la Maulamaa wa Palestina nchini Lebanon amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo nchi pekee inayounga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina na kwamba baraza hilo liko tayari kuungana na nchi zote za Kiarabu na Kiislamu kwa ajili ya ukombozi wa Palestina:

Akizungumza Ijumaa katika mahojiano na kanali ya Al Alam, Sheikh Mohammad Al Muaid Msemaji wa Baraza la Maulamaa Wapalestina nchini Lebanon, amesema, Iran haina uhasama na nchi yoyote ya Kiarabu bali inataka uhuru wa Palestina na tayari imeshapata hasara kubwa kutokana na sera zake za kuwatetea Wapalestina.

Sheikh Al Muaid ameongeza kuwa, baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kufeli mbele ya wanamapambano wa Palestina mwaka 2006 na pia kufuatia ushindi wa wanamapambano wa Palestina mwaka 2014, hivi sasa utawala huo wa Kizayuni umeingiwa na kiwewe. Ameongeza kuwa, hivi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel unapanga njama za vita vya kimadhebeu baina ya Waislamu ili kuwadhoofisha.

Wapigania ukombozi wa Palestina

Msemaji wa Baraza la Maulamaa wa Palestina nchini Lebanon amesema ulimwengu wa Kiarabu umeliuza taifa la Palestina na njama hiyo ingali inaendelea kwani Wapalestina sasa wamezingirwa katika ardhi yao na ni Iran tu inayotoa msaada kwa makundi ya wanampambano. Sheikh Al Muaid amesema hatimaye makundi ya wanamapambano Palestina yatapata ushindi.

Aidha amesema wakuu wa nchi za Kiarabu wanapapswa kusitisha mazungumzo yasiyo na faida na utawala wa Kizayuni wa Israel. Amesema pia Saudia inapaswa kusitisha vita dhidi ya watu wa Yemen na ifanye mazungumzo na Iran kwa sababu Iran ni rafiki wa mataifa yote ya Waarabu na Waislamu na kuwa adui mkuu wa ulimwengu wa Kiarabu ni utawala wa Kizayuni wa Israel.