Rais Rouhani wa Iran ampongeza Rais Kenyatta wa Kenya kwa kuchaguliwa tena
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemtumia Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ujumbe wa kumpongeza kufuatia kuchaguliwa tena kuwa rais wa Kenya.
Katika ujumbe wake siku ya Jumatatu, Rais Rouhani ameelezea matumaini yake kuwa katika duru ya pili ya urais wa Kenyatta kutashuhudiwa kuimarika uhusiano wa nchi mbili katika nyanja zote.
Aidha Rais Rouhani amemtakia Rais Kenyatta afya njema na mafanikio pamoja na ustawi wa taifa la Kenya.
Jana Mahakama ya Kilele nchini Kenya ilitupilia mbali kesi mbili zilizokuwa zimewasilishwa kupinga uchaguzi wa rais wa marudio wa Oktoba 26 na hivyo kuidhinisha ushindi wa Uhuru Kenyatta.
Majaji wote sita wa Mahakama hiyo waliafikiana kwa kauli moja katika uamuzi huo ambao sasa utaandaa mazingira ya Kenyatta kuapishwa kama rais wa Kenya, kwa muhula wa pili mfululizo, katika kipindi cha siku chache zijazo.
Mahakama ya Kilele ya Kenya imekuwa kitovu cha siasa za nchi hiyo tangu ilipobatilisha matokeo ya uchaguzi wa mwanzo wa rais uliofanyika Agosti 8 na kupelekea kufanyika uchaguzi mwingine tarehe 26 Oktoba.
Tume Huru ya Uchaguzi IEBC imefurahia uamuzi huo wa Mahakama ya Kilele na kusema ni dhihirisho la kujitolea kwa tume hiyo kufanikisha uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika.
Rais Kenyatta anatazamiwa kuapishwa Jumanne ijayo katika Uwanja wa Michezo wa Kasarani mjini Nairobi katika sherehe ambayo inatazamiwa kuhuhuduriwa na viongozi wa kieneo pamoja na wawakilishi wa nchi mbali mbali duniani.