Ripoti mpya ya IAEA yathibitisha kufungamana Iran na makubaliano ya JCPOA
Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) kwa mara nyingine tena umethibitisha katika ripoti yake mpya ya msimu kuwa Iran imetekeleza majukumu yake kuhusu makubaliano ya JCPOA.
Yukia Amano Mkurugenzi Mkuu wa IAEA ametangaza leo wakati wa kuanza kikao cha Bodi ya Magavana ya wakala wa IAEA mjini Vienna kuwa Iran imetekeleza majukumu yake kuhusu makubaliano hayo.
Yukia Amano ameongeza kuwa wakala wa IAEA ungali unaendelea kuthibitisha na kusimamia utendaji wa Iran mkabala na makubaliano ya JCPOA. Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia aidha amebainisha kuwa hadi kufikia sasa wakala huo umeyazuru maeneo yote ambayo ilihitajia kuyafikia.
Wakala wa IAEA tarehe 13 mwezi huu ulitoa ripoti yake mpya ya msimu na kuthibitisha kwa mara ya tisa kwamba Iran imefungamana na kutekeleza masharti yote kuhusu makubaliano hayo ya nyuklia yakiwemo yale yanayohusiana na kiwango cha akiba ya maji mazito, kiwango cha urutubishaji na kuwepo urani iliyorutubishwa.
Makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 linalounwa na Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani pamoja na Ujerumani yameanza kutekelezwa tangu mwezi Januari mwaka jana, hata hivyo serikali ya Marekani ikiwa moja ya nchi wanachama wa kundi hilo imekuwa ikikwepa kutekelezaji makubaliano hayo.