Mar 24, 2016 15:08 UTC
  • Larijani alaani mashambulizi ya kigaidi ya Brussels

Spika wa Majilisi ya ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran amelaani mashambulizi ya kigaidi ya juzi katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels, ambapo watu zaidi ya 30 waliuawa.

Katika ujumbe wake kwa Siegfried Bracke, Rais wa Bunge la Wawakilishi la Ubelgiji, Ali Larijani ametuma salamu za rambirambi kwa Bunge, Serikali na taifa la Ubelgiji kwa ujumla kutokana na hujuma hiyo ya kigaidi. Larijani amesema: “Hujuma hiyo ya kigaidi kwa mara nyingine tena imeonyesha udharura wa mataifa yote kuungana ili kulishinda jinamizi la ugaidi na kwamba inahitajika nguvu na umoja wa jamii ya kimataifa kukabiliana na magaidi, wafadhili na waungaji mkono wao.” Kadhalika Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu ameashiria kuwa moja ya malengo ya Jamhuri ya Kiislamu kama mhanga wa mashambulizi ya kigaidi, ni kupambana na tatizo la ugaidi na kusisitiza kuwa, Iran itaendelea kushirikiana na nchi ambazo ziko tayari kulitokomeza jinamizi hilo.

Awali Rais Hassan Rouhani wa Iran na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu Muhammad Javad Zarif walilaani mashambulizi hayo ya Brussels. Aidha taasisi na jumuiya mbalimbali za Kiislamu zimelaani vikali mashambulizi hayo ya kigaidi yaliyolenga uwanja wa ndege na kituo cha treni ya chini kwa chini mjini Brussels na kusema kuwa, mashambulizi hayo yamefanywa na wahalifu na wauaji wasio na chembe ya huruma.

Tags