Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza atembelea Iran asisitiza kuheshimu JCPOA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Boris Johnson leo amekutna na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif hapa mjini Tehran na kusisitiza kuwa London inasisitiza kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya Iran yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA).
Johnson ameongeza kuwa mapatano ya JCPOA yana umuhimu mkubwa kwa Uingereza. Halikadhalika ametaka kuimarishwa ushirikiano na uhusiano baina ya Iran na Uingereza.
Katika mkutano huo, Zarif na Johnson wamebadilishana mawazo kuhusu masuala ya kiuchumi, kibiashara na kibenki pamoja na masuala ya kieneo na kimataifa.
Boris Johnson halikadhalika amekutana na kufanya mazungumzo na Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu, Bunge la Iran na baadaye pia anatazamiwa kukutana na Rais Hassan Rouhani pamoja na Ali Akbar Salehi Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran.