Salah Zawawi asifu utendaji na mtazamo wa Kiongozi Muadhamu kuhusu Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i38351-salah_zawawi_asifu_utendaji_na_mtazamo_wa_kiongozi_muadhamu_kuhusu_palestina
Balozi wa Palestina hapa mjini Tehran amesifu utendaji na mtazamo wa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na Palestina na makundi ya harakati ya Palestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 31, 2017 14:50 UTC
  • Salah Zawawi asifu utendaji na mtazamo wa Kiongozi Muadhamu kuhusu Palestina

Balozi wa Palestina hapa mjini Tehran amesifu utendaji na mtazamo wa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na Palestina na makundi ya harakati ya Palestina.

Salah Zawawi amezungumzia uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa muqawama na mapambano ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel na kueleza kwamba, taifa la Palestina daima linatambua na kuthamini mapenzi ya serikali na wananchi wa Iran katika kuunga mkono harakati na mapambano ya wananchi wa Palestina.

Balozi wa Palestina hapa mjini Tehran amezitaka nchi zote za Kiislamu kuwasaidia wananchi wa Palestina ili waweze kuzitetea na kuzihami ardhi za Kiislamu na hivyo kuzuia mipango ya utawala ghasibu wa Israel ya kuendelea kufanya uvamizi katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muuadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa mstari wa mbele katika kuliunga mkono na kulitetea taifa madhulumu la Palestina na hilo limethibitika wazi kupitia misimamo yake katika asasi za kimataifa katika Umoja wa Mataifa.

Aidha hivi karibuni wakati Rais Donald Trump wa Marekani alipoitangaza Beitul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala ghasibu wa Israel na kutoa amri ya kuanza mchakato wa kuhamishiwa mjini humo ubalozi wa Washington kutoka Tel Aviv, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo iliyokuwa nchi ya kwanza kulaani hatua hiyo na kuitaja kuwa, inakinzana wazi wazi na maazimio ya kimataifa.