Iran yasambaratisha mtandao wa magaidi wa Munafiqina (MKO) magharibi mwa nchi
(last modified Sat, 06 Jan 2018 03:01:17 GMT )
Jan 06, 2018 03:01 UTC
  • Iran yasambaratisha mtandao wa magaidi wa Munafiqina (MKO) magharibi mwa nchi

Idara ya Usalama katika mkoa wa Lorestan magharibi mwa Iran imetangaza habari ya kusambaratishwa mtandao wa kundi la kigaidi la Munafiqina (MKO) katika mji wa Borujerd kufuatia oparesheni maalamu ya maafisa usalama wa Iran.

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Usalama ya Iran katika mkoa wa Lorestan, mtandao huo wa magaidi wa MKO ulihusika katika ghasia za hivi karibuni mkoani humo hasa katika mji wa Borujerd.

Taarifa zinasema watu wanne katika mtandao huo wa kigaidi wamekamatwa na wengine wawili walijeruhiwa katika mapigano yaliyojiri wakati wa operesheni ya kutiwa mbaroni.

Katika siku kadhaa zilizopita baadhi ya watu kwenye miji kadhaa nchini Iran walifanya mikusanyiko na maandamano kulalamikia masuala mbalimbali ikiwemo kutojulikana hatima ya watu waliopata hasara na kupoteza fedha zao katika taasisi za fedha, ughali wa baadhi ya bidhaa na udhaifu wa serikali katika usimamiaji na uendeshaji mambo.

Maandamano ya wananchi wa Iran kuunga mkono mfumo wa Kiislamu na kupinga vibaraka wa kigeni waliozusha fujo humu nchini

Hata hivyo baadhi ya maandamano hayo yalitumiwa vibaya na watu wenye nia mbaya na wahuni wanaoungwa mkono na baadhi ya nchi za Magharibi, za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel kuzusha fujo na machafuko.

Kufuatia fitina hiyo, tokea siku ya Jumatano, wananchi wa Iran kwenye miji mbalimbali wamekuwa wakishiriki katika maandamano makubwa ya kulaani njama hizo za maadui na wahuni waliotumia fursa hiyo kuharibu mali za umma.