Larijani: Ni jukumu la nchi za Kiislamu kufanya juhudi za kupunguza hitilafu
(last modified Mon, 15 Jan 2018 14:26:53 GMT )
Jan 15, 2018 14:26 UTC
  • Larijani: Ni jukumu la nchi za Kiislamu kufanya juhudi za kupunguza hitilafu

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria njama za maadui waliokula kiapo dhidi ya Uislamu kwa ajili ya kupenya na kuzusha hitilafu miongoni mwa Waislamu na kusisitiza kwamba, ni jukumu la nchi za Kiislamu kuzuia kuenea hitilafu na mizozo katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Dakta Ali Larijani amesema hayo leo pambizoni mwa mkutano wa Jumuiya ya Mabunge ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC katika mazungumzo yake na Khaled Bin Hilal Al-Mawali, Spika wa Bunge la Oman na kubainisha kwamba, kuna nyuga nyingi za kupanuliwa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Tehran na Muscat na kwamba, kuna haja ya kufanyika juhudi maradufu kwa ajili ya kufanikisha hilo.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran inayachunguza vyema mapendekezo ya Oman kuhusiana na miradi mbalimbali na kwamba, karibuni hivi itaandaa uwanja na mazingira ya utekelezaji wake.

Maspika wa Mabunge ya Iran na Oman wakiwa katika mazungumzo

Dakta Larijani amezungumzia pia suala la uwekezaji na kubainisha kwamba, kuna haja ya kurahisisha mazingira ya uwekezaji vitega uchumi hapa nchini.

Kwa upande wake Khaled Bin Hilal Al-Mawali, Spika wa Bunge la Oman amesema katika mazungumzo hayo kwamba, nchi yake inaendelea kufanya mazungumzo na Iran kwa shabaha ya kupendekeza mikakati chanya yenye lengo la kuyapatia ufumbuzi matatizo yaliyopo katika eneo hili la Mashariki ya Kati.

Mkutano wa 13 wa siku mbili wa Mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC unaanza kesho Jumanne hapa mjini Tehran na utafunguliwa kwa hotuba ya Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags