Ugaidi hauna mustakabali Mashariki ya Kati
Afisa mwandamizi wa Iran amepongeza ushindi wa hivi karibuni wa jeshi la Syria dhidi ya magaidi wa ISIS (Daesh) katika mji wa Kihistoria wa Palmyra na kusema makundi ya kigaidi hayana mustakabali Mashariki ya Kati.
Katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Al Alam, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya nchi za Kiarabu na Kiafrika, Hossein Amir-Abdollahian amelipongeza taifa la Syria kufuatia kukombolewa mji wa Palmyra kutoka katika makucha ya magaidi wa ISIS.
Amesema Syria itaendelea kupambana na magaidi na kuongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuunga mkono vita dhidi ya ugaidi Syria, Iraq pamoja na nchi zote zinazokabiliwa na tishio la ugaidi duniani.
Amir-Abdollahian ameendelea kusisitiza kuwa kuna haja ya kuwa na jitihada za pamoja za kieneo na kimataifa kukabiliana na ugaidi. Ametahadahrisha kuwa iwapo hatua hazitachukuliwa, basi ugaidi utadhuru pande zote.
Jana jeshi la Syria liliukomboa mji wa kihistoria wa Palmyra kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la ISIS baada ya mapambano ya siku kadhaa.
Itakumbukwa kuwa, Juni mwaka jana 2015, wanachama wa kundi la kitakfiri la Daesh walibomoa makaburi mawili ya kale ya Mawalii wa Allah katika mji wa kihistoria wa Palmyra mkoani Homs nchini Syria. Mkurugenzi wa Turathi za Kale nchini Syria, Maamoun Abdulkarim, alisema kuwa magaidi hao wa kitakfiri walilipua mabomu ndani ya majengo ya makaburi ya Mohammad bin Ali wa kizazi cha binamu yake Mtume Muhammad SAW na Nizar Abu Bahaaeddine, msomi mtajika wa Kiislamu kutoka Palmyra.