Bahram Qassemi ajibu tuhuma za Saudia na Misri dhidi ya Iran
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Bahram Qassemi sambamba na kutupilia mbali tuhuma za kujikariri dhidi ya taifa hili zilizotolewa katika ripoti ya pamoja ya Saudia na Misri, amesema kuwa tuhuma hizo hazina msingi, ni za kubuni na ni makosa haribifu ya kukaririwa.
Inafaa kuashiria kuwa Misri na Saudia mwishoni mwa safari ya Mohammad Bin Salman Al Saud, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia mjini Cairo, zimetoa taarifa ya pamoja zikiituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika taarifa hiyo pande hizo zimedai kuwa eti Iran inaingilia masuala ya ndani ya nchi za Kiarabu huku zikisisitizia juu ya udharura wa kushirikiana zaidi kwa ajili ya kile zilichokisema kuwa ni kuzuia uingiliaji huo wa Tehran katika nchi za Kiarabu.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbali na kukosoa hatua hiyo ya pamoja kati ya Saudia na Misri dhidi ya taifa hili amesema kuwa, kukaririwa tuhuma zisizo na msingi kutoka kwa baadhi ya nchi za eneo dhidi ya Tehran, kunatokana na kushindwa nchi hizo kukabiliana na uhalisia wa mambo ndani ya eneo na dunia kwa ujumla. Ameongeza kuwa, badala ya jumbe za kidiplomasia za nchi hizo kujadili namna ya kutatuliwa matatizo yanayozikabili nchi zao na namna ya kujikwamua na kinamansi kinachotishia mataifa hayo kusambaratika, zimekuwa zikijikita tu katika kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya nchi nyingine za eneo.
Aidha Bahram Qassemi amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikizipa nchi jirani kipaumbele cha udugu katika siasa zake za kigeni kama ambavyo pia imekuwa ikifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kutatuliwa matatizo ya eneo la Mashariki ya Kati.