Qassemi: Bin Salman ni mwanagenzi anayeona ndoto za mchana
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu matamshi yaliyojaa dharau ya Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia na kusema matamshi hayo ya Muhammad bin Salman hayana thamani ya kujibiwa kwa sababu ni mwanagenzi anayeona njozi na asiyejua lolote isipokuwa kusema uongo.
Bahram Qassemi ameyasema hayo kujibu matamshi yaliyotolewa na Bin Salman ambaye Alkhamisi ya jana alidai katika mahojiano yake na televisheni ya CBS ya Marekani kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo daima inafanya jitihada za kutatua matatizo ya kanda ya Mashariki ya Kati na kuwa na uhusiano mwema na jirani kuwa, ni "nchi hatari".
Bin Salman pia amesema, kama Iran itatengeneza bomu la nyuklia, Saudi Arabia pia itatengeneza bomu hilo haraka iwezekanavyo.
Madai hayo yasiyo na msingi ya Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran yametolewa wakati Umoja wa Mataifa, Baraza lake la Usalama na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) zimesisitiza mara kadhaa kwamba, miradi ya nyuklia ya Iran inafanyika kwa malengo ya amani.
Mwana wa mfalme wa Saudia pia amedai kuwa, jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si kati ya majeshi tano makubwa zaidi katika Ulimwengu wa Kiislamu na kwamba uchumi wa Saudia ni mkubwa zaidi ya uchumi wa Iran.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu madai hayo akisema: Jamhuri ya Kiislamu inaheshimu nchi zote jirani, nchi za dunia na mataifa yote bila ya kujali ukubwa wa nchi, uwezo wake wa kijeshi na kiuchumi na itibari yake ndani na nje.
Bahram Qassemi amesema kuwa matamshi yaliyojaa hasira na yasiyo na mantiki ya Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia yanakumbusha kipindi cha ujahilia wa mabedui. Amesisitiza kuwa, ilikuwa bora kwa nchi ambayo imelazimishwa kupiga magoti mbele ya watu wanaozingirwa kwa zaidi ya miaka mitatu na wasio na silaha wa Yemen kuzungumzia uwezo wake wa kijeshi na kiuchumi na kufunga mdomo mbele ya wakubwa wake na nchi yenye nguvu kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.