Zarif: Saudia inaendelea 'kukamwa' kwa kutoleshwa fidia na Trump
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i42666-zarif_saudia_inaendelea_'kukamwa'_kwa_kutoleshwa_fidia_na_trump
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Mtindo wa rais wa Marekani wa 'kuikama' Saudi Arabia unaendelezwa bila kusita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 04, 2018 22:56 UTC
  • Zarif: Saudia inaendelea 'kukamwa' kwa kutoleshwa fidia na Trump

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Mtindo wa rais wa Marekani wa 'kuikama' Saudi Arabia unaendelezwa bila kusita.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter kufuatia sharti lililotolewa na rais wa Marekani kwa ajili ya kuendelea kuwepo wanajeshi wa nchi hiyo nchini Syria.

Zarif ameandika: "rais wa Marekani anataka dola nyingine bilioni nne kwa wafadhili wa kifedha wa DAESH ili askari wa Marekani waendelee kuwepo nchini Syria."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefafanua kuwa, hayo yanafanywa kwa lengo la kugeuza mkondo wa mafanikio na matunda yaliyopatikana dhidi ya magaidi wenye misimamo ya kufurutu mpaka na kudhoofisha umoja wa kitaifa wa Syria.

Donald Trump, ambaye hivi karibuni alitangaza kuwa angependa kuwaondoa wanajeshi wa Marekani nchini Syria, siku ya Jumanne alitamka kwamba hatofanya hivyo kwa sharti kuwa Saudi Arabia ibebe jukumu la kuvigharimia vikosi jeshi la Marekani vilivyoko nchini humo.

Rais Donald Trump wa Marekani (kushoto) na Mfalme Salman wa Saudi Arabia

Wakati huohuo Ikulu ya Marekani White House imetangaza kuwa: jukumu la kijeshi la Marekani la kuliangamiza kundi la Daesh linakaribia kukamilika kwa kasi na kwamba kundi hilo limeangamizwa takriban kikamilifu nchini Syria.

Katika upande mwingine, afisa mmoja mwandamizi wa Marekani ambaye hakutajwa jina lake ametangaza kuwa: katika kikao cha baraza la usalama wa taifa la Marekani kilichofanyika siku ya Jumanne, Trump aliwafiki kurefushwa kwa kipindi kifupi muda wa kuwepo vikosi vya jeshi la nchi hiyo katika ardhi ya Syria.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, ushahidi na nyaraka mbalimbali zimeonyesha kuwa Washington imekuwa ikiyasaidia na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi likiwemo la ukufurishaji la Daesh katika nchi za Syria na Iraq.../