Iran: Tutatoa jibu kali iwapo Marekani itakiuka makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran amezitahadharisha nchi zinazotaka kuvuruga makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kati ya Iran na nchi 6 wanachama wa kundi la 5+1 na kusisitiza kuwa, Tehran itatoa jibu kali kwa hatua kama hiyo.
Ali Akbar Salehi amesema kuwa maadui wanapaswa kuelewa kwamba, iwapo watavuruga makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kutajitokeza hali mpya na makhsusi katika miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran.
Salehi amesema Iran haitaki kujiondoa katika makubaliano hayo na inataka kulindwa maslahi yake ya kitaifa lakini iwapo Marekani itakiuka na kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na nchi za Ulaya zikarudi nyuma na kulegeza kamba, Iran itatenda vinginevyo.
Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baina ya Iran na nchi sita za kundi la 5+1 ambazo ni Uingereza, Ufaransa, Marekani, China, Russia na Ujerumani yalitiwa saini mwaka 2015 na kuanza kutekelezwa Januari mwaka 2016. Hata hivyo serikali ya sasa ya Marekani imekuwa ikikiuka makubaliano hayo na imetoa wito wa kufanyiwa mabadiliko. Rais Donald Trump wa Marekani pia ametishia kuwa nchi yake itajiondoa katika makubaliano hayo yaliyotiwa saini na Marekani yenyewe iwapo hayatafanyiwa mabadiliko.