Iran: Madai ya Morocco kuwa tunaiunga mkono Polisario hayana msingi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i43952-iran_madai_ya_morocco_kuwa_tunaiunga_mkono_polisario_hayana_msingi
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekadhibisha vikali madai yaliyotolewa na serikali ya Morocco kwamba Tehran inawapatia misaada wapiganaji wa harakati ya Polisario inayopigania kujitenga eneo la Sahara Magharibi.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
May 02, 2018 10:54 UTC
  • Iran: Madai ya Morocco kuwa tunaiunga mkono Polisario hayana msingi

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekadhibisha vikali madai yaliyotolewa na serikali ya Morocco kwamba Tehran inawapatia misaada wapiganaji wa harakati ya Polisario inayopigania kujitenga eneo la Sahara Magharibi.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema leo Jumatano kuwa, ubalozi wa Iran nchini Morocco haujawahi kuwa na ushirikiano wala uhusiano wowote na harakati hiyo ya Polisario inayoungwa mkono na Algeria.

Qassemi ameyataja madai yaliyotolewa na serikali ya Rabat dhidi ya Tehran kuwa hayana msingi wowote, ni ghalati na yako mbali kabisa na hali halisi ya mambo. Hapo jana Morocco ilitangaza kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran kwa madai hayo ghalati.

Wapiganaji wa harakati ya Polisario ya Morocco

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, ni katika sera madhubuti za Iran kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kwamba Tehran daima imekuwa ikiheshimu uhuru wa kujitawala na usalama wa nchi nyinginezo.

Awali Muhammad Haddad, msemaji wa Harakati ya Ukombozi wa Sahara Magharibi Polisario alikanusha madai yaliyotolewa na serikali ya Morocco kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawapatia misaada wapiganaji wa harakati hiyo na kusisitiza kuwa, tuhuma hizo za serikali ya Rabat ni za bandia na ni uongo mtupu.

Hapo jana pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco, Nasser Bourita alidai kuwa harakati ya Hizbullah ya Lebanon inawapa mafunzo wapiganaji wa Polisario katika eneo la Sahara Magharibi, tuhuma ambazo zimekadhibishwa na harakati hiyo ya muqawama inayosisitiza kuwa, zimetolewa kwa mashinikizo ya Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia.