Shamkhani: Kuvunjika makubaliano ya JCPOA hakutainufaisha Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i44222-shamkhani_kuvunjika_makubaliano_ya_jcpoa_hakutainufaisha_marekani
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesisitiza kuwa kuvunjika kwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hakutakuwa na manufaa kwa Marekani; na akatoa indhari pia kwa mwenendo wa nchi za Ulaya wa kutaka kujipatia fursa zaidi kwa Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2018 12:33 UTC
  • Shamkhani: Kuvunjika makubaliano ya JCPOA hakutainufaisha Marekani

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesisitiza kuwa kuvunjika kwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hakutakuwa na manufaa kwa Marekani; na akatoa indhari pia kwa mwenendo wa nchi za Ulaya wa kutaka kujipatia fursa zaidi kwa Jamhuri ya Kiislamu.

Admeri Ali Shamkhani ametoa indhari hiyo sambamba na kukaribia kutangazwa msimamo wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusiana na makubaliano ya nyuklia maarufu kama JCPOA yaliyofikiwa kati ya Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1. Amesema ikiwa Marekani itaanzisha hatua ya kukabiliana na Iran, Jamhuri ya Kiislamu haitokaa kimya.

Akizungumzia hatua ambazo Trump anaweza kuzichukua kuhusiana na JCPOA, Shamkhani amesema: Inavyoonekana, Trump na serikali ya Marekani wanafuatilia mikakati mitatu kwa pamoja.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema, mkakati wa "kuyabakisha kwa kiwango cha chini na kuyavuruga manufaa pamoja na kuifanya JCPOA isiwe na faida yoyote kwa Iran", "kujipatia fursa zaidi kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kutumia JCPOA" na "kuiharibu JCPOA" ni mikakati mitatu ya pamoja inayofuatiliwa na Marekani kuhusiana na makubaliano hayo ya kimataifa.

Trump; mpinzani mkuu wa makubaliano ya JCPOA

Leo saa nane mchana kwa saa za Marekani, sawa na saa nne na nusu usiku kwa wakati wa hapa nchini Iran, Rais wa Marekani anatazamiwa kutangaza msimamo wa serikali ya nchi hiyo kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Tangu wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani hadi sasa, Trump amewahi kuahidi mara kadhaa kuwa ataichana hati ya makubaliano hayo, lakini hadi sasa ameshindwa kuitekeleza kivitendo kauli yake hiyo kutokana na mwafaka wa kimataifa wa kuyaunga mkono makubaliano ya JCPOA.../