Bunge la Iran lalaani hatua ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya JCPOA
Wabunge katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, wameitaka serikali ya Iran itekeleza Kipengee cha 3 cha Sheria ya Hatua Mkabala Kuhusuaiana na Utekelezwaji Mapatano ya Nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA).
Katika kikao cha leo bungeni, wabunge wametoa taarifa na kulaania vikali hatua ya Rais wa Marekani kuindoa nchi hiyo katika mapatano ya JCPOA. Wamebaini kuwa: "Rais wa Marekani ameiondoa nchi yake katika mapatano ya JCPOA kinyume cha sheria za kimataifa na ameonyesha kuwa nchi hiyo, utawala wa Kizayuni na baadhi ya tawala za Kiarabu na munafikina wote wako katika mrengo ulio dhidi ya taifa la Iran."
Katika taarifa, wabunge wa Bunge la Iran wameongeza kuwa: "Hakuna shaka kuwa kuna mtihani mkubwa kwa walimwengu hasa nchi za Ulaya zilizofikia mapatano ya JCPOA, Russia na China. Je, zitaweza kukabiliana na sera za kujitakia makuu za rais wa Marekani ili kwa njia hiyo kuwepo maingiliano mema duniani au zitaunga mkono sera za utumiaji mabavu za rais wa Marekani?"
Kwa mujibu wa Kipengee cha 3 cha Sheria ya Hatua Mkabala Kuhusiana na Utekelezwaji Mapatano ya JCPOA serikali ya Iran inapaswa kuchukua hatua za kukabiliana na kutofungamana upande wa pili na mapatano hayo katika kadhia ya kuondoa vikwazo.
Jana usiku Rais wa Marekani alitangaza uamuzi wa upande mmoja wa kuiondoa nchi yake katika mapatano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA.
Hatua hiyo ya Marekani imepingwa na nchi tatu za Ulaya za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ambazo zimetoa taarifa ya pamoja zikisisitiza kufungamana na mapatano hayo ya nyuklia.
Mapatano ya nyuklia yalifikiwa Julai 14 mwaka 2015 baina ya Iran na wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani China, Russia, Uingereza, Ufaransa na Marekani pamoja na Ujerumani. Mapatano hayo yalianza kutekelezwa mwezi Januari mwaka 2016 ambapo Iran ilipunguza baadhi ya shughuli zake za nyuklia mkabala wa kuondolewa vikwazo ilivyokuwa imewekewa kutokana na mpango wake wa nyuklia wenye malengo ya amani. Rais Trump wa Marekani amekuwa akipinga vikali mapatano hayo yalioafikiwa na serikali iliyotangulia nchini humo.