Velayati: Dhamana imara ichukuliwe kutoka nchi za Ulaya kuhusu mapatano ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i44758-velayati_dhamana_imara_ichukuliwe_kutoka_nchi_za_ulaya_kuhusu_mapatano_ya_nyuklia
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amesema: "Mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ni kuwa, katika mazungumzo na nchi za Ulaya kunapaswa kupatikane dhamana imara ili mapatano ya nyuklia ya JCPOA yasivurugike."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 20, 2018 10:18 UTC
  • Velayati: Dhamana imara ichukuliwe kutoka nchi za Ulaya kuhusu mapatano ya nyuklia

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amesema: "Mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ni kuwa, katika mazungumzo na nchi za Ulaya kunapaswa kupatikane dhamana imara ili mapatano ya nyuklia ya JCPOA yasivurugike."

Akizungumza na waandishi habari mjini Tehran leo Jumapili Ali Akbar Velayati ameashiria kuhusu nchi za Ulaya kutoa dhamana ya utekelezaji wa mapatano ya nyuklia ya Iran yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA) ambayo Marekani imejiondoa na kusema: "Ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinatoa matamshi yanayokinzana kuhusu JCPOA  na jambo hilo limeibua shaka. Kwa msingi huo timu ya mazungumzo ya Iran inapaswa kuchukua dhamana imara."

Baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza mnamo Mei 8 kuwa nchi yake imejindoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran, nchi za Umoja wa Ulaya, pamoja na China na Russia zilifanya mkutano na Iran Mei 15 na 16 kuhusu kuendelea kutekelezwa mapatano hayo pasina kuwepo Marekani. Imepangwa kuwa Mei 26 kamati ya pamoja ya JCPOA itakutana Vienna katika ngazi ya wataalamu kujadili mapatano hayo. Kumekuwepo na wasiwasi kuhusu  ahadi zinazotolewa na nchi tatu za Ulaya yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuhusu utekelezwjai wa JCPOA.

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa pia ameashiria uchaguzi wa bunge nchini Iraq na kusema uchaguzi huo umefanyika kwa usalama na watu wa nchi hiyo hawataruhusu madola ajinabi yaingilia masuala yao ya ndani. Amesema uchaguzi huo hulikuwa muhimu kwa Iran na kwamba Tehran inawatakia Wairaqi mafanikio na usalama kamili. Uchaguzi wa bunge la Iraq ulifanyika Jumamosi 12 Mei ambao watu milioni 11 walishiriki au asilimia 44 ya wapiga kura wote.