Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu kuhusu undumakuwili wa nchi za Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i45708-mtazamo_wa_kiongozi_muadhamu_kuhusu_undumakuwili_wa_nchi_za_magharibi
Ayatullahil Udhma Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumapili katika mkutano wake na mamia ya wahadhiri wa vyuo vikuu na wasomi kutoka taasisi mbali mbali za utafiti nchini alibainisha nafasi ya juu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2018 06:07 UTC
  • Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu kuhusu undumakuwili wa nchi za Magharibi

Ayatullahil Udhma Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumapili katika mkutano wake na mamia ya wahadhiri wa vyuo vikuu na wasomi kutoka taasisi mbali mbali za utafiti nchini alibainisha nafasi ya juu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa kimataifa.

Akibainisha  kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi ya juu mionogni mwa wananchi wa mataifa mengi alisema: "Iran ya Kiislamu ina maadui zaidi miongoni mwa madola ya kiistikbari kama ambavyo ina ushawishi na uungaji mkono mkubwa miongoni mwa wananchi katika mataifa ya eneo. Jambo hilo limepelekea  maadui khabithi na wa daima watekeleze njama dhidi ya taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu lakini kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu wataendelea kufeli."

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu ameashiria sera na mwenedo wa undumakuwili wa madola makubwa yanayotumia mabavu ambayo yanaunga mkono tawala vamizi ambazo zimepelekea kulazimishwa vita na kuenea ugaidi na ukaliwaji mabavu sambamba na kuenea ukosefu wa amani katika eneo na dunia.

Mtoto  Mpalestina aliyeuawa Ghaza katika hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel

Mauaji ya wanawake na watoto wa Ghaza na kuwa wakimbizi zaidi ya Wapalestina milioni tano ni ukweli mchungu wa kihistoria ambao hadi sasa unaendelea kulisibu taifa linalodhulumiwa  la Palestina.

Kuhusiana na hili, Ayatullah Khamenei ameashiria safari ya hivi karibuni ya barani Ulaya ya waziri mkuu  wa utawala wa Kizayuni (Netanyahu) ambaye ni muuaji watoto na kumtaja kuwa Shimr wa zama hizi ambaye anajionyesha kuwa amedhulumuwa na kuongeza kuwa: "Mtenda jinai huyo ambaye ni kinara wa dhulma zote katika historia amewahadaa wakuu wa Ulaya kuwa eti Iran inataka kuwaangamiza Mayahudi milioni kadhaa katika hali ambayo pendekezo letu la utatuzi wa kadhia ya Palestina ni la kimantiki kabisa na ni mantiki inayoenda sambamba na demokrasia."

Hakuna shaka kuwa, kadhia ya Palestina si kadhia pekee katika Ulimwengu wa Kiislamu lakini ni kigezo cha kupima  madai ya haki za binadamu na kuheshimiwa sheria za kimataifa.

Kadhia ya Palestina ina nukta mbili ambazo haziwezi kupingika.

Nukta ya kwanza: Haki zilizokanyagwa za taifa la Palestina zinapaswa kurejeshwa.

Nukta ya pili: Kumeshuhudiwa uzembe wa jamii ya kimataifa, hasa Umoja wa Mataifa na nguzo yake muhimu yaani Baraza la Usalama, katika kutekeleza majukumu yake ya kukabiliana na utawala ghasibu na vamizi wa Israel na kutetea haki za Palestina. Ni jambo la kusikitisha kuwa taasisi za kimataifa zimenyamazia kimya masaibu ya Palestina na zimeafiki kutumiwa kama chombo cha kufikia malengo haramu ya madola makubwa ya kibeberu na vamizi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa kimya cha nchi za Ulaya kuhusu jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ghaza na kusema: "Daima tumekuwa tukisema kuwa, ili kuainisha serikali katika nchi ya kihistoria ya Palestina kunapaswa kutumiwa mbinu ambayo walimwengu wote wanaiafiki  yaani kufanyike kura na uchunguzi wa maoni  yenye kuwahusisha Wapalestina wote halisi ambao wako ndani au nje nchi ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu wawe ni Waislamu, Mayahudi au Wakristo ambao kwa uchache miaka 80 iliyopita walikuwa katika ardhi hizo"

Ayatullah Khamenei ameashiria ukweli huo na kuongeza kuwa: " Je, pendekezo hilo la Jamhuri ya Kiislamu, ambalo  limesajiliwa rasmi katika Umoja wa Mataifa linaendana na vigezo vya kimantiki vinayokubaliwa duniani au la? basi kwa nini nchi za Ulaya haziko tayari kufahamu hilo?

Saudia inawaua watoto wa Yemen kwa uungaji mkono wa madola ya Magharibi

Jibu la swali hilo na makumi ya maswali mengine yenye madhumuni kama hiyo linapatikana katika sera za undumakuwili  za watawala wa nchi za Magharibi ambao wanahadaa wanapodai kuwa wanatetea haki za binadamu au demokrasia. Isisahaulike kuwa jinai mbaya zaidi katika historia zimetekelezwa na madola hayo hayo ya Magharibi yanayotoa nara za uongo za eti kutetea haki za binadamu. Tawala ambazo hivi sasa zinawaua watoto kiholela, yaani tawala za Israel na Saudi Arabia, zenyewe zimetokana na hii harakati chafu ya kupinga ubinadamu.

Katika matukio hayo yaliyojaa machungu, ni wazi kuwa kimya cha wenye kudai kutetea haki za binadamu ambao wana taasisi zinazoweza kukabiliana na jinai za utawala haramu wa Israel huko Ghaza, kimepelekea kuendelea dhulma ya kihistoria dhidi ya taifa la Palestina.