Korea Kaskazini yakerwa na matamshi machafu ya Netanyahu dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i45738-korea_kaskazini_yakerwa_na_matamshi_machafu_ya_netanyahu_dhidi_ya_iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini ametoa radiamali kuhusiana na pendekezo la kejeli la Waziri Mkuu wa Utawala haramu wa Kizayuni kuhusu kuipa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran teknolojia ya kukabiliana na uhaba wa maji na kusema kuwa, Benjamin Netanyahu ni mtenda jinai na muongo mkubwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 12, 2018 04:17 UTC
  • Korea Kaskazini yakerwa na matamshi machafu ya Netanyahu dhidi ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini ametoa radiamali kuhusiana na pendekezo la kejeli la Waziri Mkuu wa Utawala haramu wa Kizayuni kuhusu kuipa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran teknolojia ya kukabiliana na uhaba wa maji na kusema kuwa, Benjamin Netanyahu ni mtenda jinai na muongo mkubwa.

Ri Yong-ho Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Korea Kaskazini aliyasema Jumatatu kupitia ujumbe alioutuma katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, Netanyahu ametoa pendekezo hilo la dharau dhidi ya Iran la eti kutaka kuipatia nchi hii teknolojia hiyo ya maji, katika hali ambayo utawala wa Kizayuni haujawahi kutoa msaada wowote kwa nchi hata moja duniani ghairi ya kufanya jinai tu.

Ri Yong-ho Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Korea Kaskazini

Kadhalika Ri Yong-ho ameashiria mgogoro uliopo katika eneo la Ukanda wa Gaza ambao unasababishwa na mzingiro uliowekwa kwa miaka kadhaa sasa na utawala huo katili wa Kizayuni dhidi ya raia wa eneo hilo na kubainisha kwamba, badala ya Netanyahu kuliokoa eneo la Gaza kutokana na uhaba wa maji, ndio kwanza huwa anawaua kila siku wakazi wake kwa silaha angamizi. Jumapili iliyopita Waziri Mkuu wa utawala huo wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu alitoa pendekezo la kejeli dhidi ya Jamhuri ya Kislamu ya Iran kwa kudai kwamba Israel itaipatia Tehran teknolojia inayohusiana na kukabiliana na uhaba wa maji kwa lugha ya Kifarsi kupitia tovuti. Kufuatia matamshi hayo machafu, Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran sambamba na kuashiria jinai za utawala wa Kizayuni katika kuwaua raia wasio na hatia wa Palestina, amemtaka Netanyahu kuacha mara moja jinai hizo dhidi ya Wapalestina na jinai nyingine nyingi za kivita zinazofanywa na utawala wake bandia na kusisitiza kwamba Iran kwa kutegemea utaalamu wake wa ndani itaweza kutatua tatizo la uhaba wa maji nchini.

Bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Ameongeza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejiweka tayari kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la uhaba wa maji na kamwe haitohitajia msaada wa utawala huo unaotenda jinai. Naye kwa upande wake Issa Kalantari, Mkuu wa Shirika la Kuhifadhi Mazingira la Iran amejibu pendekezo hilo la dharau la Netanyahu, kwa kusema, badala ya Netanyahu kujiingiza katika masuala yasiyomuhusu ya nchi hii, anatakiwa atoe majibu kuhusiana na jinai zinazomkabili yeye na utawala wake katili dhidi ya raia madhlumu wa Palestina.