Larijani: Iran itachukua hatua muafaka kukabiliana na chokochoko za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i45766-larijani_iran_itachukua_hatua_muafaka_kukabiliana_na_chokochoko_za_marekani
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, Ali Larijani ameashiria hatua ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA, na kusema: 'Hatua hii ya Marekani imeathiri kwa kiasi fulani uwekezaji nchini, na ili kukabiliana na hilo, tayari hatua maufaka zimechukuliwa na mazungumzo yanaendelea."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 12, 2018 09:38 UTC
  • Larijani: Iran itachukua hatua muafaka kukabiliana na chokochoko za Marekani

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, Ali Larijani ameashiria hatua ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA, na kusema: 'Hatua hii ya Marekani imeathiri kwa kiasi fulani uwekezaji nchini, na ili kukabiliana na hilo, tayari hatua maufaka zimechukuliwa na mazungumzo yanaendelea."

Akizungumza na waandishi habari mjini Tehran leo asubuhi, Larijani amesema: "Kwa kuzingatia kuwa Marekani ilikiuka maadili, sheria na ahadi zake kimataifa kuhusiana na JCPOA na kisha ikajiondoa rasmi katika mapatano hayo, kuna udharura wa kuwepo mpango maalumu na sahihi wa kukabiliana na Marekani."

Larijani aidha amesema, hatua zilizochukuliwa na Marekani dhidi ya Iran si jambo jipya kwani uhasama huo ulianza tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.

Itakumbukwa kuwa Jumanne usiku tarehe 8 Mei, 2018, Rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuitoa nchi yake kwenye mapatano ya JCPOA licha ya kwamba Washington ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha wakati wa urais wa Barack Obama. Nchi zingine tano zilizoafiki mapatano ya JCPOA, zikiwemo za Ulaya zimesisitiza kubakia katika mapatano hayo.

Rais Trump wa Marekani

Mnamo Mei 23, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei alibainisha masharti ya Iran kuendelea kubakia katika JCPOA na kusisitiza kuwa: "Nchi za Ulaya zinapaswa kuwasilisha azimio dhidi ya Marekani katika Baraza la Usalama, ziahidi pia kuwa kadhia za makombora na ushawishi wa Iran katika eneo hazitajadiliwa na pia zikabiliane na vikwazo vyovyote vya Marekani dhidi ya Iran." Aidha Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa nchi za Ulaya zinapaswa kutoa dhamana ya kununua mafuta ya Iran kwa kiwango ambacho Iran inahitaji na pia benki za Ulaya zinapaswa kutoa dhamana ya kutekeleza malipo ya kifedha kwa ajili ya biashara na serikali pamoja na sekta binafsi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.