Zarif arejea Tehran kutokea Afrika Kusini
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amerejea hapa Tehran leo asubuhi baada ya kumaliza ziara rasmi nchini Afrika Kusini ambako alionana na kufanya mazungumzo na viongozi wa mbalimbali wa nchi hiyo.
Jumanne wiki hii, Mohammad Javad Zarif aliwasili mjini Pretoria akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi wa Iran katika ziara ya kikazi nchini Afrika Kusini ambako ameonana na waziri mwenzake wa mambo ya nje pamoja na Rais Cyril Ramaphosa wa nchi hiyo.
Maudhui kuu iliyojadiliwa na pande mbili katika ziara hiyo ni suala la mapatano ya nyuklia ya JCPOA, masuala ya uchumi na njia ya kustawishwa zaidi ushirikiano wa nchi mbili katika nyuga tofauti.
Katika ziara hiyo kumefanyika pia kikao cha kiutaalamu baina ya Iran na Afrika Kusini ambacho kimejadili masuala ya kiuchumi na mawasiliano na uchukuzi pamoja na kutafutwa njia za kurahisisha utoaji visa kwa raia wa nchi mbili.
Afrika Kusini ni nchi ya pili kwa kuwa na uchumi mkubwa barani Afrika na imechukua hatua nzuri za kuimarisha uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari mjini Pretoria, Zarif alisema juzi Jumanne kuwa, Afrika Kusini ni moja ya washirika wa karibu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwamba serikali ya nchi hiyo daima imekuwa ikiunga mkono haki za wananchi wa Iran katika kadhia ya nyuklia kuanzia mwanzo wa mazungumzo hadi baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA.