Sera za Marekani zimepelekea kuendelea migogoro katika eneo
Mwenyekiti wa Tume ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, amesema: Sera za kivita na za kuunga mkono makundi ya kigaidi zinazotekelezwa na Marekani sambamba na hatua ya nchi hiyo kukiuka mikataba ya kimataifa hasa mapatano ya nyuklia ya Iran, JCPOA, ni chazo cha kuendelea migogoro katika eneo."
Alaeddin Boroujerdi aliyasema hayo Jumamosi mjini Tehran wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na mbunge kutoka Georgia, Shalva Kiknavelidze ambaye ni mwenyekiti wa Kundi la Urafiki la Mabunge ya Iran na Georgia. Huku akibainisha masikitiko yake kuhusu hali mbaya ya kibinadamu nchini Yemen, Boroujerdi amesema: "Mauaji ya watoto wasio na hatia, wanawake na raia nchini Yemen ni matokeo ya uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani kwa Saudia Arabia."
Mwenyekiti wa Tume ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni katika Bunge la Iran ameongeza kuwa baada ya miaka mitatu ya mapambano na muqawama, watu wa Yemen, wakiwa na suhula duni sana, wameweza kuwapa pigo kubwa la kijeshi wavamizi Wasaudi na waitifaki wao.
Boroujerdi ameashiria sera za kimsingi za Iran za kupambana na ugaidi na kusema: "Maendeleo yanahitaji usalama endelevu na ushirikiano wa nchi zote duniani katika vita dhidi ya ugaidi."
Hali kadhalika Boroujerdi amesema Georgia na Iran zinaweza kuimarisha uhusiano katika nyanja mbali mbali za kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi.
Kwa upande wake, Shalva Kiknavelidze Mwenyekiti wa Kundi la Urafiki la Mabunge ya Iran na Georgia amesema kutumiwa uwezo wa kiuchumi wa nchi za eneo kunahitaji kwanza kuwepo amani na usalama na kwa msingi huo kuna udharuria wa kuimarishwa uhusiano wa Tehran na Tblisi.