Iran: Mapatano ya nyuklia ya JCPOA bado yako hai
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, licha ya kwamba Marekani imejitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA lakini makubaliano hayo ya kimataifa bado yako hai na mazungumzo juu ya namna ya kuendeleza ushirikiano kupitia mapatano hayo yangali yanaendelea.
Bahram Qassemi amesema hayo leo Jumatatu na kuongeza mbele ya waandishi wa habari wa ndani na nje na kuongeza kuwa, mapatano ya JCPOA hivi sasa yako imara.
Amesema, rais wa Marekani, Donald Trump ameuonesha ulimwengu namna Wamarekani wasivyo na mwamana kwa kujitoa katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu swali la mwandishi wa Radio Tehran kuhusiana na mazungumzo baina ya Russia na Saudia juu ya kuongeza kiwango cha uzalishaji mafuta na nafasi ya kitengo cha uchumi cha Wizara ya Mambo ya Nje tya Iran katika mazungumzo hayo amesema, ijapokuwa OPEC na masuala yanayohusiana yanashughulikiwa na Wizara ya Mafuta na wizara hiyo huwa inafanya kazi zake vizuri katika uwanja huo, lakini Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kila inapolazimu huwa inabadilishana mawazo na Russia kuhusu kuongeza kiwango cha uzalishaji mafuta cha OPEC.
Amezungumzia pia mgogoro wa Yemen na kuongeza kuwa, daima Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikilaani uvamizi wa Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu. Ameongeza kuwa, hivi sasa Yemen imeingia kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa na kwamba jamii ya kimtaifa na nchi za Ulaya zina wajibu wa kuchukua hatua za haraka za kukomesha mgogoro huo.